Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini kuunda na kuenzi tunu za Taifa na kuhakikisha wanajukumu la kuja na Falsafa na Moyo wa kukuza Uzalendo Miongoni mwa Watanzania.
Wakili Mpanju amesema hayo katika siku ya pili ya Kikao kazi cha Maafisa Maendeleo ya Jamii Novemba 09, 2022 jijini Dodoma.
Mpanju amesema Shabaha kuu ya kukuza Uzalendo ni kuongeza na kuendeleza Mila na desturi kwa makusudi ya kuimarisha Taifa kwa kizazi kijacho.
“Kwa mnaokumbuka kilichokuwa IDM Mzumbe hiki ni moja ya Vyuo vilivyokuwa vikiwapika Viongozi kwa kusudio la kuwafanya kuamsha ari ya Uzalendo miongoni mwa Watanzania” amesema Wakili Mpanju.
Hata hivyo Wakili Mpanju amesema kuanzia Miaka ya 1990 hali ya Uzalendo imeendelea kulegalega nchini kutokana na watu kupoteza Uzalendo na kutokuwa na mapenzi na Nchi yao.
“Katika miaka hiyo ya 1990 kumekuwepo na Mila na Desturi ambazo zipo kinyume na tamaduni zetu katika mavazi, miziki na hata mtindo wa Maisha umebadili kabisa na kupotosha Mila hali iliyo didimiza Uzalendo wa Watanzania” alisema Wakili Mpanju
Hata hivyo Wakili Mpanju amewataka Maafisa Maendeleo kuwa vinara kwakuandaa Miongozo itakayo saidia kukuza Uzalendo kwenye jamii na kuwataka Maafisa Maendeleo kuvitumia Vyuo na Taasisi za Maendeleo ya Jamii kwa kuandaa Mada na kuziwasilisha katika Majukwaa tofauti ikiwepo Vyuo, Vyombo vya Habari na Mikutano mbalimbali ya hadhara.
Akichangia Mada wakati wa wasilishao hilo Afisa Maendelo ya Jamii Mkoa wa Lindi Gaudence Nyamwihula alisema tunu za Taifa zinapolindwa zinasadia kuchochea maendeleo ya Nchi pamoja na kulinda undugu, uwajibikaji pamoja na Mshikamano.