Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk Rose Reuben amesema tatizo la rushwa ya ngono katika maeneo ya kazi linazidi kuota mizizi.
Wakati nchi ya Tanzania ikiungana pamoja na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, wadau wa masuala ya jinsia wameitaka Serikali kuridhia mkataba wa kimataifa unapingana na rushwa ya ngono sehemu za kazi kwa maana imezidi kukithiri zaidi ya hapo awali.
Kwa mujibu wa wadau hao, changamoto ya rushwa ya ngono imekuwa ikikua kila pachao huku wanawake na watoto wa kike wakiwa ndiyo wahanga wakubwa katika hilo.
Dk. Rose Reuben amesema “Tulifanya utafiti kuangalia rushwa ya ngono kwenye vyombo vya habari, tukabaini huko hali ni mbaya na bahati mbaya ni kwamba hawazungumzi. Kati ya waliohojiwa asilimia 52 hawakuwa wazi kusema kuhusu hilo,”
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili wa kijinsia (Mkuki), Wakili Anna Kulaya amesema mkataba huo wa kimataifa utasaidia kuweka msimamo wa Serikali dhidi ya vitendo hivyo.
“Huu mkataba sio mbaya na hauna athari yoyote kwetu ndiyo maana tunaomba Serikali iuridhie ili tuwe na njia na mwongozo wa pamoja wa kukabiliana na changamoto hii,” amesema Anna.