
Serikali imesema imekuwa ikiwalipa Waheshimiwa Madiwani wa Mamlaka za Serikali za Mitaa posho ikiwemo Halmashauli ya Mji wa Makambako kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Sura 287 na 288 kwa kuzingatia kanuni za kudumu za Halmashauli husika.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dkt Festo Dugange jana 7 Novemba 2022 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Makambako Mhe. Deo Sanga akitaka kujua ni lini Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Makambako wataongezewa posho kama ilivyo katika Halmashauri nyingine.
Dugange amesema kuanzia mwaka 2019 Halmashauri ya Makambako imekuwa ikilipa posho ya vikao shilingi 50,000 ikiwa ni shilling 10,000 zaidi ya kiwango kilichopendekezwa, hivi sasa viwango vya posho za safari kwa Halmashauri hiyo vinalipwa kwa kuzingatia waraka wa zamani kwa sababu viwango vya posho mpya havikutengewa bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa kuwa mabadiliko ya posho yametoka wakati bajeti ya Halmashauri ilikuwa imekwishaandaliwa na kupitishwa kwenye vikao vya kisheria na maamuzi.
Aidha, Dugange amesema Halmashauri ya Mji wa Makambako inashauriwa kufanya mapitio ya bajeti au izingatie maelekezo ya waraka Namba moja ya Utumishi wa Umaa wa tarehe 10 Juni, 2022 kuhusu posho za kujikimu kwa safari za kikazi ndani ya nchi kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha .
Pia amesema kwa mwaka huu wa fedha Serikali Kuu imechukuwa jukumu la kulipa fedha za posho za Madiwani katika Halmashauri zetu na Serikali inafanya tathimini ya kuona uwezekano na uwezo wa Serikali wa kuongeza posho hizo ili muda ukifika posho ziongezeke kwa ajili ya Waheshimiwa Madiwani.
ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT