Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema katika kuhakikisha wanafikia malengo ya kukusanya mapato kwa wenye nyumba za kupanga, wako katika mchakato wa kushirikiana na TAMISEMI kuzitambua na kuziingiza kwenye mfumo maalumu nyumba hizo za kupanga kwa lengo la kukusanya kodi inayostahili.
–
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar Es Salaam, Charles Bajungu aliyemwakilisha Kamishna wa Kodi za Ndani amesema wamebaini kuwepo kwa ukwepaji wa kodi hiyo kwa kiwango kikubwa huku sababu mojawapo ikiwa ni kukosekana kwa takwimu mahsusi ya nyumba hizo nchini.
–
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Uledi Abbas Mussa amesema katika kuonesha shukrani zao kwa walipakodi bora, wameamua kutoa Tuzo kwa wadau hao, hafla inayotarajiwa kufanyika leo November 17, 2022.
–
Aidha amesema, kwa mwaka wa fedha 2022, TRA imefanikiwa kuvuka lengo la asilimia 14.6 walilojiwekea kwa kukusanya takribani shilingi trilioni sita kwa mwezi Julai hadi Septemba ikiwa ni lengo la ufanisi kwa asilimia 100.5.