
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wadau wote duniani kuona umuhimu wa wanaume kushiriki vita dhidi ya ukatili wa kijinsia unaowaathiri zaidi wanawake na watoto.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Wanawake na Haki uliofanyika Jijini Instabul, Uturuki tarehe 5 Novemba, 2022 wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Akitoa salaam za Rais Samia, Waziri Dkt. Gwajima ameishukuru Serikali ya Uturuki kwa mwaliko wa mkutano huo wenye Kaulimbiu ya Kanuni za Kimataduni na Wanawake (Cultural Codes and Women), amesema maendeleo ya kijamii na vizazi siyo suala la wanawake tu ni la jamii yote.
Waziri Dkt. Gwajima ameeleza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuwezesha maendeleo yanayozingatia usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili kwa wanawake unaochangiwa na mila na desturi potofu.
Amesema, sambamba na kuendelea kutelekeza makubaliano ya kikanda na kimataifa kuhusu wanawake na maendeleo kuelekea usawa wa kijinsia wanawake wanaendelea kuwezeshwa kwenye elimu, uongozi wa kisiasa, kitaaluma na kijamii.
Amebainisha, uwiano wa uandikishaji wa watoto wa kiume na wa kike shule ya msingi kufikia 1:1 huku Serikali ikitekeleza mpango wa elimu bila ada kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Aidha, mpango wa kujenga Shule moja maalumu ya Sekondari kwa wasichana katika mikoa yote 26 nchini Tanzania kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi, teknolojia, injinia na hesabu kwa kifupi (STEM) jambo ambalo litawainua watoto wa kike kielimu.
Kwa upande wa wanawake na uongozi Waziri Dkt. Gwajima ameueleza mkutano huo kuwa, Tanzania ipo mstari wa mbele katika kuwainua wanawake. Pamoja na takwa la Katiba ya Nchi kuwa 30% ya viti vya bunge ni viti maalumu kwa ajili ya wanawake na 33.3% ni viti maalumu vya madiwani wanawake, Rais Samia ameongeza idadi ya Mawaziri kamili wanawake hadi 9 huku akiwapa kuongoza Wizara nyeti kwa maendeleo ya Taifa.
Vilevile, Mabalozi Wanawake na Majaji wanawake wameongezeka
