Kwa takribani miezi 10 Halmashauri ya wilaya ya Geita imethibitisha kuwa imepokea taarifa 26 za vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto, huku ikiwataka wanaume kutoa taarifa zao kwani wengi wao wamekuwa wakiona aibu kutoa taarifa hizo na kusababisha kukosa takwimu zilizokamilika kuhusiana na ukatili wanaofanyiwa.
Hayo yamesemwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Geita,Bi. Enedy Mwanakatwe kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, yenye kauli mbiu ya “Kila uhai una thamani”, huku baadhi ya wanaume wakielezea sababu za wao kutopata sauti zao.
“Matukio ya ukatili yaliyotolewa taarifa ni 26, katika natukio hayo, ubakaji yamekuwa ni saba, ulawiti wawili na vipigo ni 17, pamoja na matukio hayo kutolewa taarifa na wanawake na watoto, lakini pia wanaume baadhi wamekuwa ni wahanga wa ukatili japokuwa hawatoi taarifa katika ofisi zetu na hivyo kukosa takwimu zao kwa urahisi”, amesema Mwanakatwe.
Kwa upande wake mwananchi wa mkoa huo amesema, “Sisi kama wanaume tunafanyiwa sana ukatili wa kijinsia na wanawake yani wake zetu lakini unashindwa kuanzia kwamba uende wapi kwa sababu sisi huwaga hawatujali sana, mnaowajali sana ni wanawake, sasa ninashindwa kuelewa labda kwa siku ya leo kwa kuwa waandishi mmekuja mimi lazima nitoe tu ya ukweli hata sisi tunateswa sana”, alisema Mashiri.