ADVERTISEMENT
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji kwa kushirikiana na sekta binafsi ihakikishe inakamilisha taratibu za utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Rufiji utakaosambaza maji katika maeneo ya mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) iendelee kutenga fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima zaidi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maji. “Tusipokuwa makini tutaingia katika janga la ukame.”
Ametoa maagizo hayo (Jumanne, Novemba 2, 2022) baada ya kukutana na Waziri wa Maji, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Muwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na viongozi wa DAWASA kwa ajili ya kujadili hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Novemba 02, 2022 ametembelea mradi wa visima 10 vya maji vilivyopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam ambavyo vinauwezo wa kuzalisha maji lita milioni 70 kwa siku.
Akiwa katika eneo hilo la mradi, Waziri Mkuu ameitaka DAWASA kuhakikisha kuanzia leo Novemba 2, 2022 wanaingiza maji katika mfumo wa usambazaji maji kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam ili kukabiliana na uhaba wa maji kwenye jiji hilo.
Pamoja na kutembelea mradi huo, Mheshimiwa Majaliwa amewasha moja ya pampu ya visima hivyo pamoja na kufungua mfumo wa maji yanayokwenda kwa wananchi.
Hatua hii ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Novemba 01, 2022 la kuhakikisha anasimamia mradi wa maji kigamboni uanze kupeleka maji kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.


ADVERTISEMENT