
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange ameonesha kutoridhishwa na ujenzi wa zahanati ya Manchali B iliyopo Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Dkt. Dugange amefanya ziara hiyo mapema jana tarehe 06.12.2022 katika Halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma katika kijiji cha Manchali B huku akiwasisitiza Watendaji hao kuwa na utaratibu wa kujifanyia tathmini ya utendaji kazi kwani ni muda mrefu wamekaa na fedha za kuendeleza ujenzi bila sababu za msingi.
“hii ni changamoto kubwa kama tunaweza kukaa na milioni 50 ya zahanati kwa zaidi ya miezi 12 bila kukamilisha, nafikiri tunahitaji kujitathmini na kuchukua hatua, wananchi wanasubiri, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta fedha sisi kazi yetu ni kutekeleza na kuhakikisha miradi imekamilika na wananchi wanaanza kupata huduma” amesema Dkt. Dugange.
Amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt. Semistatus Mashimba kumweleza wamejipangaje ili itakapofika Desemba 12, 2022 zahanati 4 zilizopatiwa fedha ziwe zimekamilika ili ziweze kuanza kutoa huduma ya Afya kama inavyotarajiwa ambapo Mkurugenzi huyo alisema maelekezo yote wameyapokea na kwamba watayafanyia kazi ili zahanati hizo zianze kutoa huduma kwa wananchi.
Mganga Mkuu wa mkoa Dkt. Best Magoma amesema 2021/22022 mkoa ulipatiwa shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya uendelezaji zahanati katika mkoa wa Dodoma na matarajio ifikapo tarehe 30 Desemba miradi yote iwe imekamilika lakini pia katika mwaka 2022/2023 mkoa umepata shilingi milioni 550 kwa ajili ya zahanati 11 na Halmashauri ya Chamwino wamepatiwa zahanati mbili zitakazokamilishwa.
Naye Peter Athman Afisa Afya akisoma taarifa ya zahanati ya kijiji cha Manchali B ambayo imejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 93.5 amesema ujenzi wa jengo hili unahusisha nguvu za wananchi 3,522,000 ikihusisha ukusanyaji wa mawe, mchanga na kokoto, mapato ya ndani ya Halmashauri shilingi milioni 10 na shilingi milioni 50 fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kumalizia jengo la zahanati lakini kwa sasa zahanati inakabiliwa na changamoto ya nyumba ya mtumishi.
Kwa upande wake Mheshimiwa Nelson Mtundu Diwani kata ya Manchali ameishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa zahanati lakini ameiomba Serikali kuwajengea Kituo cha Afya ili kusogeza huduma kwani Kata yake inavyo vijiji vitano ambavyo havina kituo cha afya.

ADVERTISEMENT