
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema mwaka 2023 Serikali kupitia uratibu wa wizara yake inajielekeza kwenye kuimarisha na kuunganisha mifumo kuanzia ngazi ya Msingi hadi Taifa ili kuongeza nguvu ya mapambano kwenye kudhibiti na kutokomeza ukatili wa kijinsia na watoto.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo akifungua kongamano la wanawake na uongozi lenye lengo la kujadili ushiriki wa wanawake katika uongozi ili kutokomeza ukatili wa kijinsia, Desemba 02, 2022 jijini Dar es Salaam.
Amesema kuna haja ya kuzijengea uwezo endelevu Kamati za ulinzi wa wanawake na Watoto zilizopo ili zifanye kazi na wadau wa mitandao yote iliyoko kwenye jamii.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau inatambua umuhimu wa kuwa na wanawake viongozi mahiri na kuwekeza rasilimali katika usawa wa kijinsia kama chachu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia hivyo kamati hizo zikiimarishwa usawa wa kijinsia utafikiwa na kuondoa ukatili wa kijinsia.
Amebainisha kuwa Kamati za ulinzi wa wanawake na Watoto 18,186 kati ya 20,750 (asilimia 88) zimeanzishwa katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Halmashauri, Kata na Kijiji kwa mwaka 2021/22.
“Tathmini ya MTAKUWWA 2017/2022 imeonesha kupungua kwa matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa kwa asilimia 31 kutoka matukio 42,413 mwaka 2020 hadi 29,373 mwaka 2021. Matukio ya ukatili wa Watoto yamepungua kwa asilimia 28 kutoka matukio 15, 870 kwa mwaka 2020 hadi matukio 11,499 mwaka 2021, hata hivyo, tunatambua kuwa watu wengi bado hawatoi taarifa” amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Aidha, amebainisha kuwa katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo yenye usawa wa Kijinsia nchi inatekeleza Jukwaa la Kizazi chenye Usawa ambapo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara wa eneo hilo.
Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kwamba Serikali inatambua mchango mkubwa wa wanawake ambao ni zaidi ya nusu ya Watanzania wote na imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda inayoweka misingi ya usawa kwa binadamu, ambapo matokeo ya juhudi hizo ni kuona wanawake wakishika nafasi nyeti za uongozi kwa ufanisi nchini.



ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT