Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya amewaonya Wasanii wa Tanzania wanaotunga nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi na kusema hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu ya Wasanii hao.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo mapema jijini Dar es salaam amesema “Kuna Wasanii wanahamasisha matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi, kama kuna wasaniii ambao wanadhani badala ya kutunga nyimbo za kuhamasisha Jamii wao wanatunga nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya, sheria yetu inasema hao tutawachukulia hatua”
“Kama kuna Msanii anadhani anaweza kupata umaarufu kwa kupitia nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya hatutomuacha hata mara moja, sheria itachukua mkondo na ipo siku nitawaita Waandishi wa habari ili muone kitu gani tumekifanya kwa Wasanii wanaotaka kupata umaarufu kwa kutumia dawa za kulevya”
“Mbona mashairi yapo ya aina nyingi unashindwaje kutunga mashairi ya vitu vyote, si wahamasishe hata kilimo bora au biashara, kwani lazima wahamasishe mambo ya bangi? hatutoruhusu Mtanzania yoyote afanye uhamasishaji wa matumizi ya dawa za kulevya” ——- asema Kamishna Gerald Kusaya.
KonceptNewsUpdates.