ADVERTISEMENT
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wanaosaidia watoto waishio katika mazingira magumu kwani wanasaidia ajenda ya kupunguza wimbi la watoto hao na madhara yake.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo akizungumza katika mahafali ya kwanza ya shule ya sekondari ya Shirika la Masista wa Maria, iliyopo Kisarawe, mkoani Pwani, Desemba 14, 2022.
Waziri Dkt. Gwajima amesema watoto wanaopitia mazingira magumu wanakumbana na hatari nyingi ikiwemo vitendo vya ukatili vinavyoathiri maisha yao na taifa kwa ujumla.
“Nimejiuliza hawa watoto wa kike wote 626 wangekuwa wapi muda huu bila shule hii, wengine wangepata ndoa na mimba za utotoni na mambo mengine ya changamoto nyingi, hivyo kuna haja ya kuunga mkono juhudi za wadau hawa ili watoto wengi zaidi wanaopitia maisha magumu wanufaike” amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali ina mifumo ya kuwasaidia familia zilizo na maisha magumu kupitia mfuko wa TASAF lengo ambalo hata shule hii inatekeleza hivyo vema kuimarisha uratibu ili kuongeza nguvu ya kuwasaidia ambao hawajafikiwa.
Ameipongeza shule hiyo yenye mtaala wa kipekee kwani ina mtaala wa kawaida pamoja n ule wa ufundi ambao unawasaidia watoto hasa wa kike kwa kuwapa elimu ya Sekondari pamoja na ufundi kwa wakati mmoja ili wanapotoka shule wawe na ujuzi wa kuweza kujiajiri na kuajiri wengine.
Kwa upande wake Meneja wa shule hiyo yenye wanafunzi 626 Johanitha Joramu amesema, Mahafali hayo ya kwanza yana Wahitimu 142 ambao wana ujuzi mbalimbali kama kushona, kupika na ufundi umeme.
Johanitha ameongeza kwamba, mpango wa shirika ni kuongeza shule kama hiyo kwa ajili ya watoto wa kiume, jijini Dodoma.
Naye mmoja wa wahitimu wa shule hiyo Dominista Kaitani ameshukuru kwa kupata nafasi hiyo ya kupata elimu na ujuzi kwani wengi wao walikuwa hawajui hatima ya maisha yao kutokana na ugumu wa maisha.
Mahafali hayo pia yamehudhurwa na Mwadhama Kadinali Polycarp Pengo aliyeongoza ibada ya misa takatifu kabla na kushiriki kugawa vyeti vya taaluma kwa wahitimu.
ADVERTISEMENT