
Wadau wote wanaopambana na ukatili wa kijinsia nchini wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na mpango
kazi katika kutekeleza majukumu yao ya kutokomeza ukatili wa jinsia na watoto.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipokuwa akihitimisha kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na maadhimisho ya Kimataifa ya Haki za Binadamu yaliyofanyika mkoani Dar es salaam Desemba 10,2022.
Waziri Dkt. Gwajima amewataja wadau hao kama majeshi ya kupambana na ukatili wa jinsia na watoto kuwa ni pamoja na Kamati za MTAKUWWA, NGOs, SMAUJATA, Skauti, Girls Guide, Redcross, Mabaraza ya Wazee na Watoto, Mitandao ya Wanawake pamoja na taasisi za kivyama hususan wanawake, vijana na wazazi, viongozi wa dini na wengine wote kwa ujumla.
Amesema Taasisi zote hizo zinafika kwenye jamii hivyo amezitaka zifikishe na ujumbe wa sauti ya kupiga vita ukatili na katika kumalizia kampeni hiyo ni kuashiria kwamba matukio ya ukatili wa kijinsia ni ukiukwaji wa haki za Binadamu
Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kuwa moja ya majukumu yake ni kuratibu utekelezaji wa wadau katika kukomesha machozi ya wanawake na watoto na kwamba katika kutekeleza Kampeni hii ya Siku 16 ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia na kwa Watoto alikuwa anatekeleza agizo la Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kunakuwa na ushiriki mpana katika ngazi za wilaya hadi mtaa na kwamba, maagizo hayo yataishi daima ili kuchochea mapambano endelevu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto.
“Ninatangaza vita endelevu dhidi ya wote wanaojihusisha na matendo ya ukatili wa aina hii kwamba wasalimu amri”
“Wadau tuungane kutokomeza hili, tungefanya tathimini ya wapi pa kupeleka rasilimali na nguvu kutokana na uhitaji basi eneo hili ndiyo lingehitaji uwekezaji mkubwa kwani ndiyo linaongoza kwa uvunjifu wa haki za binadamu” amesema Mhe. Dkt. Gwajima.
Aidha, amesema, takwimu zinaonyesha, vitendo vya ukatili wa kijinsia ndiyo uvunjifu wa haki za binadamu uliokithiri zaidi duniani na anatumaini kuona ongezeko la uwekezaji katika afua za ukatili wa kijinsia.

