ADVERTISEMENT

Mhe. Mwanaidi amesema hayo alipokua akijibu hoja katika kikao kazi kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii na Wizara ya Maendeleo Ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Januari 23, 2023 Jijini Dodoma.
Naibu Waziri Mwanaidi ameihakikishia Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge kuwa Wizara itaunda timu itakayoweza kubaini chanzo halisi cha ukatili maana elimu peke yake haitoshi kutatua changamoto hii ya ukatili nchini.
“Tunahitaji kuchukua hatua za haraka zitazotatua changamoto hii kikamilifu ndio maana kama Wizara tumeamua kuja na mbinu hii ya kuunda timu ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tatizo la ukatili katika jamii ” alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mheshimiwa Stanslaus Nyongo ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuhakikisha inashirikiana na Wizara ya Elimu, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara zote za kisekta ili kurahisha utatuzi wa janga la ukatili nchini.
“Wizara inabidi ifanyie kazi suala la Udhibiti wa Vitabu vinavyosomwa na Watoto kwani kuna maudhui yanayoharibu na kupotosha watoto na kuchochea ukatili katika jamii kwani vitu wanavyojifunza vinachochea kufanyiana ukatili wao kwa wao“ alisema Nyongo.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amesema Wizara inaendelea kutatua changamoto ya upungufu wa Maafisa Ustawi nchini katika kuhakikisha wanaongeza nguvu katika kupambana na vitendo vya ukatili hasa katika kutoa huduma kwa manusura na wahanga wa vitendo vya ukatili.
“Katika hili la kuongeza Maafisa Ustawi wa Jamii nchini tutashirikiana na wadau mbalimbali ili kuongeza nguvu zaidi katika kupambana na vitendo vya ukatili” alisema Dkt. Chaula
Dkt. Chaula ameongeza Serikali pia inaendelea kuhakikisha inatoa huduma za Malezi kwa wazee wasio na ndugu.


ADVERTISEMENT