
Serikali imetenga shilingi Trilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi zenye uchakavu kupitia mradi wa kuimairisha elimu ya msingi na awali (Boost).
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki jana tarehe 10 Januari, 2023 mkoani Pwani wakati akizungumza na Maafisa Elimu Wilaya na Kata, Wakuu wa Shule za Sekondari na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na viongozi wa Elimu ngazi ya Halmashauri wakati wa kikao kazi cha Uboreshaji wa Usimamizi wa Elimumsingi na Sekondari katika viwanja vya shule ya sekondari kibaha.
Waziri Kairuki amesema tathmini ya kina inaendelea kufanyika chini ya Ofisi yake ili kujua uchakavu wa miundombinu ya shule za msingi ambapo baada ya tathmini hiyo kuna shule ambazo zitapata ukarabati mkubwa, ukarabati mdogo na nyingine kuvunjwa kabisa kwa kuwa hazikidhi viwango vya kutolea elimu.
“katika kuimarisha miundombinu ya elimu ya awali na msingi kupitia mradi wa BOOST, tumetenga jumla ya shilingi Trilion 1.15 ambazo zitatumika katika ujenzi na ukarabati wa shule katika kipindi cha miaka 5 na kwa kuanzia kwa mwaka huu wa fedha tutaanza na shilingi Bilioni 259 ” amesema Kairuki.
Aidha, Waziri Kairuki alifanya ziara fupi kujionea ujenzi wa madarasa katika shule ya sekondari Sofu iliyopo Mji wa Kibaha ambayo ujenzi wake umekamilika na wanafunzi wamekwisha anza masomo kidato cha kwanza.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa mkoa wa Pwani Mheshimiwa Abubakar Kunenge amesema mkoa wake ulifanya tathmini na kuona baadhi ya mila za wananchi sio nzuri hasa kwa watoto wa kike ambapo wameanza kuchukua hatua na kuanzisha kampeni za kumuokoa mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na wazazi kuwekewa mazingira salama majumbani na shuleni.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya rais TAMISEMI bw. Vicent Kayombo amesema kuwa kikao kazi hicho cha Uboreshaji wa Usimamizi wa Elimumsingi na Sekondari kina lengo la kuweka uelewa wa pamoja ili kuboresha elimu msingi nchini lakini pia Serikali imeendelea kujenga madarasa ya shule za msingi na sekondari kote nchini.


ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT