Mbunge wa Ulyankulu (CCM), Rehema Migilla ametaka kampuni za simu katika jimbo lake ambayo yamekuwa yakitoa huduma zenye kasi ndogo kuwafidia wananchi.
Akiulizwa Swali lihusianalo na huduma za mawasilano katika kikao cha Bunge leo Februari 6,2023 ametaka Serikali kutolea ufafanuzi zaidi namna inawasaidia wananchi kutokana na adha inayowakumba katika upande wa mawasiliano.
“Je, hizi kampuni za simu ziko tayari kuwafidia hawa wananchi wetu ambao fedha zao zimetumika bila kupata huduma kwa sababu huu ni wizi kama wizi mwingine,”amehoji Rehema.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Methew Kundo amesema minara iliyopo katika maeneo hayo katika kata ya Nhwande inauwezo wa 2G pekee yake haijaanza kutoa huduma ya 3G.
Amesema mpango ni kuiboresha kufikia 3G hadi 4G na kwamba wakifikia katika kiwango hicho huduma itaweza kutolewa bila shida yoyote.
Hiyo inalenga zaidi kuwasaidia watumimiaji wa huduma za mawasiliano kufurahia spidi nzuri ya mtandao popote walipo kupitia huduma zinazotolewa na kampuni husika.