ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT
Uongozi wa Klabu ya Yanga umetangaza kusikitishwa na tamko lililotolewa na Mdhamini wake mkuu ‘SportPesa’ likiishutumu Klabu hiyo kukiuka makubaliano ya kimkataba kwa kuzindua jezi maalumu ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la CAF yenye nembo ya Mdhamini mwingine “Haier”.
–
Muongozo wa CAF kuhusiana na klabu zinazoshiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho la CAF kwenye hatua ya makundi unazuia matumizi ya udhamini wa kampuni za michezo ya ubashiri “Betting”.
Uongozi wa Yanga uliwajulisha SportPesa juu ya matumizi ya nembo ya Haier, kama mbadala wa udhamini kwenye mashindano ya CAF.
–
Kwa kuwa, Mdhamini wetu mkuu SportPesa anazuiwa kikanuni kwenye mashindano ya CAF, mkataba kati ya Yanga na SportPesa hauizuii Klabu ya Yanga kutafuta Mdhamini mbadala kwenye nafasi hiyo, hivyo basi Klabu ikaamua kuingia makubaliano ya udhamini na Kampuni ya Haier kwa ajili ya mashindano ya CAF pekee. Kwa maelezo hayo, Klabu inathibitisha kuwa haijavunja kipengele chochote cha mkataba wake na SportPesa.
–
Mnamo saa 1:52 usiku wa tarehe 30 Januari, 2023, siku ya uzinduzi wa jezi maalumu kwa ajili ya michuano ya CAF zenye nembo ya Mdhamini Haier, Klabu ilipokea barua pepe kutoka kwa Mdhamini wetu mkuu SportPesa, wakiielekeza klabu kutumia nembo ya “Visit Tanzania” kwenye nafasi ya mbele ya jezi kwa ajili ya mashindano ya CAF na ikiishinikiza klabu kuhudhuria uzinduzi wa jezi hizo siku inayofuatia, tarehe 31, Januari 2023, saa 5:00 asubuhi kwenye ofisi zao.
–
Klabu ya Yanga ilitafsiri maamuzi haya ya SportPesa ni kitendo kisicho na mantiki na chenye dhamira ovu na kinachokiuka makubaliano ya kimkataba kwa pande zote mbili.
–
Klabu ya Yanga inatambua kwamba, nembo ya “Visit Tanzania” sio chapa wala mpango wa Mdhamini wetu SportPesa, hivyo tusingeweza kutumia nembo hiyo bila maridhiano na mmliki wa nembo hiyo.
–
Klabu inapenda kuujulisha umma kuwa, hatujatafutwa na taasisi yoyote kuhusiana na matumizi ya nembo ya “Visit Tanzania” hivyo hatukukataa kutumia nembo hii kama ilivyoelezwa na SportPesa.