Uvutaji sigara ni tabia mbaya inayoweza kusababisha madhara makubwa kwa afya yako, Madhara haya yanaweza kuwa ya muda mfupi au ya muda mrefu, na yanaweza kusababisha magonjwa mbalimbali hatari.
–
Kwa bahati mbaya, watu wengi huanza kuvuta sigara bila kujua madhara yake na kisha wanashindwa kuacha. Katika makala hii, tutazungumzia juu ya madhara ya uvutaji sigara na jinsi ya kuacha.
–
Kuna Kemikali zaidi ya 4,000 ndani ya Sigara ambazo zinaweza kudhuru mwili wa Mvutaji, Na kila sekunde 8, mtu mmoja hufariki dunia kutokana na matumizi ya Tumbaku (source: Wikipedia)
–
Madhara ya Uvutaji Sigara:
1.Kusababisha matatizo ya kupumua
Sigara ina kemikali nyingi hatari ambazo zinaweza kusababisha uharibifu wa mapafu na kupunguza ubora wa pumzi. Hii inaweza kusababisha shida ya kupumua au kuleta matatizo mbali mbali kama vile pumu na kifua kikuu.
2.Kusababisha saratani ikiwemo Saratani ya mapafu(Lung cancer)
Uvutaji sigara ni sababu kubwa ya saratani ya mapafu. Sigara na tumbaku vina kemikali hatari kama vile nikotini na karboni monoksaidi ambazo zinaweza kusababisha uharibifu wa seli za mapafu na kusababisha saratani.
3. Kusababisha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu
Sigara ina kemikali nyingi hatari ambazo zinaweza kusababisha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu. Kemikali hizi zinaweza kusababisha kufunga kwa mishipa ya damu na kupunguza mtiririko wa damu kwenye moyo na viungo vingine vya mwili.
4. Kusababisha kupungua kwa nguvu za kiume
Uvutaji sigara unaweza kusababisha kupungua kwa nguvu za kiume. Sigara ina kemikali ambazo zinaweza kusababisha kupungua kwa mtiririko wa damu kwenye sehemu za uzazi ikiwemo kwenye Uume, Hii inaweza kusababisha tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.
NB; Kuna Kemikali zaidi ya 4,000 ndani ya Sigara ambazo zinaweza kudhuru mwili wa Mvutaji, Na kila sekunde 8, mtu mmoja hufariki dunia kutokana na matumizi ya Tumbaku (source: Wikipedia)
5. Tatizo la nywele kunyonyoka
Hii ni kutokana na kwamba,uvutaji wa Sigara hudhoofisha kinga ya mwili na kupelekea mizizi ya nywele za Mvutaji kudhurika.
6. Kusababisha Magonjwa ya Macho,
Tafiti zinaonyesha kwamba sehemu ya macho inayopunguza mwanga inaweza kufunikwa na kitu kama vile Wingu,hivo kusababisha hali ya upofu wa macho kwa Mvutaji wa Sigara.
7. Matatizo ya Ngozi,
Athari katika Ngozi hutokana na kemikali zilizopo kwenye Sigara, Hapa huhusisha ngozi kukuchanjamana, kwani kemikali hizo hupunguza uwezo wa ngozi kujirekebisha na kusababisha ngozi kuzeeka haraka na kupoteza uwezo wa kulainika.
8. Magonjwa ya Masikio,
Sigara huweza kusababisha uwepo wa uchafu ambao huganda kwenye Mishipa ya Damu,hivo kupunguza uwezo wa damu kutembea ndani ya Sikio,na kuleta matatizo katika maskio ya mvutaji ikiwemo tatizo la kutokuskia Vizuri.
9. Saratani ya Ngozi,
Kemikali zilizopo ndani ya Sigara huweza kusababisha Vidonda kwenye ngozi kutokupona haraka, na kueguka kuwa Saratani katika Ngozi.
10. Magonjwa ya meno,
Sigara huweza kuongeza uchafu ambao unaganda kwenye Meno hivo kupelekea meno kuoza pamoja na harufu mbaya mdomoni.
11. Magonjwa ya Mapafu,
Sigara huweza kusababisha Saratani ya mapafu,pamoja na Koromeo(koo), na pia kupasuka kwa vifuko vya hewa Ndani ya mapafu.
12. Matatizo ya Mifupa,
kemikali ndani ya Sigara huweza kudhoofisha mifupa na kupunguza Nguvu katika mifupa.
13. Magonjwa ya Moyo,
Uvutaji wa sigara huweza kusababisha,tatizo la shinikizo la Damu(Presha), mshtuko wa moyo,na kusababisha kifo pia.
14. Tatizo la Vidonda vya tumbo,
Hii ni kutokana na kwamba,kemikali ndani ya sigara hupunguza uwezo wa tumbo kustahimili Acid baada ya kula,hivo kupelekea tatizo la Vidonda vya tumbo.
15. Madhara kwenye vidole,
ikiwemo tatizo la kutu katika kucha na Vidole vya Mvutaji.
16. Ugonjwa wa Buerger,
Huu ni uvimbe wa Mishipa ya Damu miguuni na mikononi ambapo tatizo hili lisipotibiwa haraka hupelekea kukatwa Mguu au mkono.
Jinsi ya Kuacha Uvutaji Sigara:
✓ Tafuta msaada wa kitaalamu
Kuacha uvutaji sigara ni ngumu sana. Ni muhimu kutafuta msaada wa kitaalamu ili kukusaidia kufanikiwa,
Unaweza kumtafuta daktari wako au mshauri wa afya ili kukuongoza kwa njia sahihi ya kuacha uvutaji sigara.
✓ Fikiria juu ya faida za kuacha uvutaji sigara
Ni muhimu kuwa na motisha wa kutosha wa kuacha uvutaji sigara,huku ukifikiria zaidi kuhusu faida za kuacha kuvuta Sigara.
✓ Punguza matumizi ya sigara
Badala ya kuacha ghafla, unaweza kuanza kwa kupunguza matumizi ya sigara hatua kwa hatua,
Kwa mfano, unaweza kuanza kwa kuvuta sigara chache tu kwa siku, na kisha kupunguza taratibu hadi kuacha kabisa.
✓ Tafuta njia mbadala za kupunguza msongo wa mawazo
Wakati mwingine watu hutumia sigara kama njia ya kupunguza msongo wa mawazo.
Badala yake, unaweza kutafuta njia mbadala za kupunguza msongo wa mawazo kama vile;
- Kufanya mazoezi kama yoga,kukimbia, kutembea n.k,
- au kufanya vitu unavyovipenda zaidi n.k
✓ Ondoa vitu vinavyokufanya uvute sigara
Ikiwa kuna vitu ambavyo vinakufanya au kukushawishi uvute sigara kama vile pombe au marafiki wako wa zamani, jaribu kuondoa vitu hivyo katika maisha yako au jaribu kubadilisha mazingira yako ili kuzuia kutaka kuvuta sigara.
✓ Jitunze wewe mwenyewe
Kuacha uvutaji sigara kunaweza kuwa ngumu sana kwa mwili na akili yako,
Ni muhimu kuhudumia vizuri mwili wako na akili yako, Unaweza kujitunza wewe mwenyewe kwa kula lishe bora, kufanya mazoezi, na kupata usingizi wa kutosha.
–
Chanzo : Afyaclass