Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Tanga, limefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu wanne raia wa Cameroon, ambao wamedai wapo nchini Tanzania kwa ajili ya kufanya majaribio ya kujiunga na timu za Coastal Union na African Sports zilizopo jijini Tanga.
–
Kwa mujibu wa Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Tanga, Kagimbo Bakari, wahamiaji haramu hao wamedai wameletwa na wakala aitwaye Benard Matomondo Mfaume.
–
Hata hivyo alibainisha kuwa mara baada ya kuwakamata raia hao, waliwaita viongozi wa timu za African Sports na Coastal, ambao walikana kuwatambua wala kuwa na mawasiliano nao na barua walizokuwa nazo zote ni za kughushi na pasipoti walizokuwa nazo sio sahihi.
–
“Uchunguzi wa awali unaonyesha raia hawa wa Cameroon waliingia kupitia uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere JKNIA na kupata viza za matembezi ya siku 90 na sio za kufanya shughuli zozote za michezo na wapo hapa tayari kwa kufanya mazoezi ili waweze kisajiliwa katika timu hizo za Coastal Union na African Sports” alisema Kamanda Bakari.