ADVERTISEMENT
Mhariri Mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Oni Sigala amewataka Watanzania kupuuza bango la kughushi linalozunguka katika mitandao ya kijamii likisema Baraza hilo limekemea vikali matumizi ya maneno ya ‘famchezo nini, famasihara nini na fautani nini ambayo kwa siku za karibuni yamekua yakitumika na baadhi ya Watu mitandaoni.
–
Taarifa rasmi ya Baraza hilo imeeleza yafuatayo “si kweli na Baraza halihusiki na bango hilo lenye makosa mengi ya kiuandishi lakini makosa makubwa zaidi aliyoyafanya Mwandishi ni kuonya matumizi ya misimu aliyoorodhesha ambayo kimsingi baraza halijawahi kukemea au kuonya matumizi ya maneno ya misimu”
–
“Tunapenda kuwakaribisha Wadau wote wa Kiswahili wenye nia ya kuelimisha jamii kupata ufafanuzi wa kina kwa jambo wanalotaka jamii ijifunze, pia tunawaomba wanaoghushi nembo na nyaraka za Baraza kuacha mara moja kwa kuwa ni kosa kisheria kutumia nembo na nyaraka bila idhini ya baraza”
–
“Matumizi ya misimu yanaweza kukuza lugha iwapo yatakuwa na mashiko na yatasanifiwa, Baraza linaomba kupuuzwa kwa mabango ambayo yanatengenezwa na Watu wachache wasio waaminifu kwa lengo la kujiongezea wafuasi katika kurasa zao” imeeleza taarifa hiyo.
ADVERTISEMENT