Golikipa wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini na klabu ya Kaizer Chiefs, Emile Baron amepokea msaada wa kiasi cha pesa zaidi ya Milion 245 kutoka kwa mashabiki wa klabu yake ya zamani ya Lillestrøm ya Norway baada ya kufahamishwa kuhusu hali ya kusikitisha ya mchezaji huyo aliyestaafu.
Baron alicheza soka la kulipwa mara ya mwisho katika mechi kati ya Bidvest Wits dhidi ya Orlando Pirates alipovunjika mguu tarehe 27 Aprili 2013. Tangu wakati huo ameangukia katika umaskini na kuhangaika kutafuta riziki kwa mke wake na wanawe wawili.
Baron alikiri kwamba mambo yalikuwa mabaya sana alijaribu kujiua mara nne, mara ya mwisho mnamo Novemba mwaka jana 2022 kutokana na maisha kuwa magumu, pia alifukuzwa kutoka kwa nyumba ndogo ya chumba kimoja na kulala barabarani
“Mambo ni mabaya zaidi sasa. Mimi na mke wangu tumekuwa tukilala barabarani, watoto wanaendelea vizuri hadi sasa,” Baron aliandika kupitia SMS na kutuma TV 2 ya Norway
Waliposikia habari za kusikitisha kuhusu hali ya Baron, mashabiki wa Lillestrøm, klabu ambayo Baron aliichezea kati ya 1999 na 2005, walitoa wito wa kuwepo kwa mchango mkubwa nchini Norway, huku michango ikitoka kwa karibu watu 5,000.
“Kuna watu wengi wamesikitishwa sana kusikia hali ya Emile anavyoishi sasa. Watu wengi, wengi wanaotaka kuchangia,” Morten Stokstad, meneja w habari na mawasiliano wa Lillestrøm aliiambia TV 2 baada ya klabu hiyo kuungana na kundi rasmi la mashabiki wanajiita “Kanari-Fansen”.
Baron, alionekana kushangakwa kiasi kikubwa cha uungwaji mkono aliopokea kiasi hiko cha pesa kwa kusema “Sina la kusema. Sijui jinsi ya kutoa shukrani zangu, ni kubwa sana. Asante sana,” aliambia TV 2 kwenye SMS nyingine.
Takriban Kr1,1 Milion ( sawa na Shilling Milion 243 za Kitanzania) zilikusanywa kutoka kwa mashabiki na watu wa Lillestrøm kote nchini Norwe, kama ilivyoripotiwa na TimesLIVE.
Baron alifunguka kuhusu matatizo yake ya kifedha mwaka wa 2019, akisema hakupokea pesa za bima kutoka kwa PSL baada ya jeraha lake. Pia alisema vilabu vya ndani havikujibu maombi yake ya usaidizi.
Mchezaji huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 43 alianza uchezaji wake katika klabu ya Hellenic mwaka wa 1996, kabla ya kuhamia Lillestrøm baada ya kurejea Afrika Kusini, alichezea Kaizer Chiefs kati ya 2005 na 2009. Kisha akajiunga na SuperSport United kwa misimu miwili, kabla ya miaka miwili akiwa Bidvest Wits kabla ya jeraha lake la mwisho la soka.
Alishinda ubingwa wa Ligi Kuu Afrika Kusini akiwa na SuperSport mnamo 2009/10 na kuiwakilisha Bafana Bafana mara sita, ikijumuisha mara mbili kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika la 2004.
NB : Hili ni somo na funzo kwa wachezaji wetu wa Tanzania kujikatia bima ya Afya ni muhimu sana katika kipindi cha uchezaji wako, pia ni muhimu sana kwa mchezaji kuondoka katika klabu vizuri kwa nidhamu ili hata pindi utakapopata matatizo wakuunge mkono kwa kutambua mchango wako. Pia ili soma kwa mashabiki kuthamini mchango wa wachezaji wao wa zamani. Imeandikwa na Shabani Rapwi ( Nyota wa Mchezo).