Mhudumu wa baa ya Nyemo, Kibaha mkoani Pwani, Asia Eliya (24) amefariki dunia kwa madai ya kunywa pombe kupita kiasi bila ya kula chakula.
–
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Picha ya Ndege, Joseph Zambo alisema kuwa Asia alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali.
–
Zambo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 8, mwaka huu majira ya alfajiri nyuma ya baa kwenye migomba jirani na alipokuwa akifanyia kazi.
–
“Nilipigiwa simu kuwa kuna mwili wa mtu aliyekufa ilibidi niende na nilipofika niliambiwa mwili umechukuliwa na polisi kupelekwa Tumbi ambapo alikuwa hajafa na alifia njiani,” alisema.
–
Alisema kuwa wafanyakazi wenzake walisema kuwa siku hiyo Asia alikunywa sana pombe kabla ya umauti kumkuta.
–
“Alichunguzwa lakini hakukutwa na jeraha lolote wala kuumia popote, hali ambayo inaonesha kuwa inawezekana pombe ndiyo ilisababisha kifo hicho,” alisema Zambo.
–
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo alikiri kutokea kwa tukio hilo.
–
Source: HabariLeo