Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla amewataka wamiliki wa baa, vyombo vya muziki na kumbi za starene kufuata na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ili kuepusha kero ya kelele za muziki kwa wananchi.
–
Makalla ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano uliohusisha viongozi wa Serikali za mitaa, masoko na wadau wa mazingira.
–
Amewaelekeza viongozi wa Serikali za Mitaa kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kudhibiti utoaji vibali vya ujenzi wa baa na kumbi za starehe.
–
Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam amesema kumekuwa na malalamiko kuhusu uvunjaji wa sheria kufuatia ongezeko la baa na kumbi za starehe kwenye makazi ya watu, ikiwa ni pamoja na upigaji muziki usiku kucha, jambo linalowaathiri wananchi.
–
Kwa mujibu wa sheria na kanuni za NEMC, adhabu kwa wanaokiuka sheria kwa kupiga muziki kwenye makazi ya watu ni faini ya shilingi Milioni mbili hadi milioni 10, kifungo cha miaka miwili jela au vyote kwa pamoja, na sheria inaruhusu upigaji muziki kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa nne usiku kwa kiwango kilichoruhusiwa.
–
Kwa baa ama nyumba za starehe zinazotoa huduma usiku kucha, nazo zimetakiwa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja la kuwa na vibali vinavyowaruhusu kufanya hivyo.