Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameitaka Serikali kuacha kukwepa wajibu wao kuhusu malipo ya wastaafu kwa kisingizio cha kutofikishwa michango yao.
Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 13, 2023 kufuatia mchango wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako wakati wa kuhitimisha hoja ya Waziri Mkuu kwa maombi ya fedha 2023/24.
Katika mchango wake Profesa Ndalichako amesema kuwa Serikali imekuwa ikilipa michango kwa wakati na hasa mafao kwa watumishi wanapostaafu bila kuwa na sumbufu isipokuwa kama kulikuwa na tatizo lingine.
Spika amesema kauli ya kama kulikuwa na tatizo ndiyo imekuwa ni chanzo cha kuwaumiza wastaafu hasa kucheleweshwa kwa malipo ya wastaafu wakati hawahusiki kwa lolote katika mapungufu hayo.
“Hapa kila wakati nawakumbusha, suala la kutopelekwa kwa michango ya mwajiriwa ni tatizo la mwajiri na Serikali, hivi inakuwaje michango haiendi kwenye mifuko lakini Serikali mmekaa kimya wakati mnajua kuna riba kwa mcheleweshaji badala yake mnakuja kumuumiza mwajiriwa,” amesema Dk Tulia.
Kiongozi amesema umefika wakati sasa kwa Serikali kuwa inalipa michango moja kwa moja kwa wastaafu bila kuwasumbua ili baada ya hapo wao waendelee kuwadai waajiri ambao hawakuwa wamepeleka michango hiyo.
Awali kwenye michango yao, Profesa Ndalichako aliombewa taarifa na wabunge Ester Bulaya na Halima Mdee mara kadhaa walioonyesha kupinga hoja yake kuhusu ukwasi wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo imekuwa na mapungufu hata kwenye malipo ya wastaafu.
CC; Mwananchi