Klabu ya Yanga imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2022/23, baada ya ushindi wa magoli 4-2 dhidi ya Dodoma Jiji katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Magoli ya Yanga katika mchezo huo yamefungwa na Kennedy Musonda dakika ya 38, Mudathir Yahya aliyefunga magoli mawili dakika ya 70 na 90+3′ na Farid Mussa dakika ya 87′ huku magoli ya Dodoma Jiji yakifungwa na Collins Opare dakika ya 58′ na Seif Karihe dakika ya 67′.
Huu unakuwa Ubingwa wao wa 29 na mara ya pili mfululizo, wakiwa na mechi 2 mkononi na alama zao 74 haziwezi kufikiwa na timu yoyote.
Huenda huu ndio msimu bora zaidi kwa klabu hiyo tangu kuasisiwa kwake 1935 wakiwa kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Nusu fainali ya Azam Sports Federation Cup, Ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC na walishatwaa ngao ya jamii mapema.