
Ndejembi ameyasema hayo leo Mei 15, 2023 jijini Dodoma wakati wa kufungua mafunzo elekezi kwa waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa mradi wa DART.
Amesema kutokana na majukumu ya wakala huyo ni vyema kuanza mchakato wa kufanya usanifu wa huduma hiyo katika majiji makubwa likiwemo jiji la Dodoma.
“Rai yangu kwa DART ianze kuangalia maenoe mengine kama jiji la Dodoma, mfano kwa sasa TANROADS inaanza ujenzi wa njia nne kutoka Mji wa Serikali hadi katikati ya jiji, hivyo DART mzungumze na TARURA na TANROADS ili kwenye mipango yao waweze kuweka eneo la akiba katikati ya barabara”amesema Ndejembi
Ameendelea kufafanua kua hatua ya kusanifu ikianza mapema itaondoa adha ya kuvunja vunja na kulipa fidia pindi upanuzi wa huduma hii utakapofika kwenye majiji makubwa.
Aidha, Ndejembi amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Jiji la Dar es Salaam ili kuhakikisha wananchi wanafika katika shughuli zao kwa haraka.
Akielezea utekulezaji wa Mradi wa DART kwa Jiji la Dar-es-salaam Mhe. Ndejembi amesema katika awamu ya kwanza ya mradi Serikali imetumia dola za Marekani milioni 235 wakati awamu ya pili Serikali imetenga dola za Marekani milioni 141 na utekelezaji wake umefikia asilimia 96.
Ndejembi amesema katika awamu ya tatu ya kutoka mjini hadi Gongo la Mboto, Serikali imetenga dola za Marekani milioni 148 na mkandarasi yuko eneo la kazi kuendelea na utekelezaji wa mradi.
Awali, Mkurugenzi wa Utawala, Rasilimali Watu wa DART, Dk Eliphas Mollel alisema Wakala imesaidia sana kuondoa msongamano wa abiria na kuwa kumekuwa na ongezeko la kusafirisha abiria kutoka abiria 50,000 hadi kufikia abiria 200,000 kwa kila siku.
