Kocha msaidizi wa Simba SC, Juma Mgunda alimaarufu kama Pep Guardiola Mnene (Master Game Plan) ametoa kauli nzito kwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe ambaye alimtolea maneno ya kejeli akiwa kwenye umati wa watu.
Mgunda kupitia mahojiano na Mwanaspoti amesema kwamba hata kabla ya Kamwe kumuomba msamaha, yeye alishamsamehe kwa kauli isiyokuwa ya staa aliyoitoa dhidi yake.
“Sijaonana naye ana kwa ana, lakini amenipigia simu usiku na kuniomba msamaha, lakini hata kabla hajakumbuka kufanya hivyo mimi tayari nilikwisha msamehe,” amesema Mgunda na kuongeza;
“Hata hivyo katika maisha anapaswa kukumbuka kitu kikubwa ni heshima bila kujali cheo cha mtu, ufadhili wake kwako au kumuangalia sura yake, kwani ukitoa kashfa kwa kudhamiria inakujengea mazoea na kesho au keshokutwa utamkosea mwingine na mwingine huenda akafika hadi kwa yule anayekufadhili,” amesema Mgunda