

Akiba Commercial Bank Plc imeshiriki kikamilifu katika tamasha la vijana linalojulikana kwa “Kijana Janjaruka” ambalo limeandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ambalo limeanza kuanzia tarehe 20-24 Mei, 2023 katika viwanja vya Zakhem – Mbagala.
Lengo la tamasha hilo ni:- kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa vijana wa Manispaa ya Temeke na maeneo ya jirani. Pili, kualika taasisi za fedha hususan mabenki ili kutoa elimu ya fedha kwa vijana.
Tatu, kuonyesha bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na mabenki na taasisi nyingine.
Akitembelea banda la Akiba Commercial Bank Plc katika viwanja hivyo siku ya tarehe 22 Mei, 2023 Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mheshimiwa Mwanahamisi Munkunda ambapo pamoja na mambo mengine alipata nafasi ya kufahamu fursa mbalimbali zitolewazo kwa vijana kupitia Benki ya Akiba hususan huduma za Bima za BODASURE ambayo inalenga kutoa ulinzi kwa wamiliki na waendesha bodaboda na Bajaj.
Pia, benki ya Akiba imezindua akaunti maalum kwaajili ya Wanawake inayoitwa akaunti ya WARIDI ambayo ina masharti nafuu sana ya uendeshaji, lengo ni kuwainua Wanawake katika kufikia ndoto zao za mafanikio katika ujasiriamali.
Zaidi ya hayo, Benki ya Akiba imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya fedha kwa vijana na umma kwa ujumla hususan katika nyanja ya kujiwekea Akiba, huduma za Mikopo, mpango wa fedha na kupanga bajeti za mtumizi binafsi na Biashara.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Temeke amefurahi na ameishukuru benki ya Akiba kwa kuonyesha mfano wa kuigwa kwa kutoa huduma bora jamii, pia, ameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi za fedha hususan mabenki katika kuchochea maendeleo endelevu ndani ya Manispaa ya Temeke na Taifa kwa ujumla.
Tamasha hilo linatarajia kufungwa siku ya tarehe 24 Mei, 2023 huku likikadiriwa kukusanya zaidi ya vijana laki 2 kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Temeke.