
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia na ile ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ziandae utaratibu utakaosaidia vijana kujifunza na kumfahamu zaidi hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuanzia shule za msingi, hadi vyuo vikuu.
Ametoa wito huo (Jumamosi, Mei 6, 2023) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kongamano la kumbukizi ya miaka 101 ya hayati Mwalimu Nyerere lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Amesema kuwa kama lilivyo lengo la kongamano hilo ni muhimu kuwarithisha vijana wa Kitanzania fikra na falsafa za Baba wa Taifa. “Aidha, nyote mtakubaliana nami kwamba yapo mambo mengi ambayo tungetamani vijana wetu wayafahamu kuhusu urithi aliyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.”
Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kumekuwa na taarifa za malalamiko kuhusu kuongezeka kwa kelele na mitetemo katika sehemu mbalimbali nchini na maeneo yaliyoongoza kwa kulalamikiwa ni za nyumba za starehe, kumbi za burudani na nyumba za ibada.
Amesema katika kudhibiti kelele na mitetemo kutoka katika kumbi za starehe, Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa maelekezo mahususi yaliyolenga kudhibiti mitetemo iliyopitiliza katika kumbi za starehe hapa nchini. Pia, maelekezo hayo yaliainisha jinsi uratibu unavyopaswa kufanyika katika nyumba za ibada kwa kuwaomba viongozi wa dini kupitia Kamati za Amani kujadili suala la kelele na mitetemo iliyopitiliza kutoka kwa baadhi ya nyumba za ibada ili kupata namna bora ya kuendesha shughuli za ibada.
Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema, kumejitokeza taharuki kwa baadhi ya viongozi wa dini wakati Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashughulikia malalamiko kuhusu ongezeko la kelele na mitetemo.
“Serikali ingependa kutoa ufafanuzi kwamba shughuli za dini ziendelee kufanyika kama kawaida na suala la uratibu wa jambo hilo katika nyumba za ibada liendelee kuratibiwa na viongozi wa dini wenyewe kupitia Jumuiya ya Maridhiano na Amani.”



Hisia zote:
15
ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT