Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kuongeza nguvu zaidi katika kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo mara baada ya kuongoza zoezi la kufanya usafi katika soko kuu la wamachinga mjini Dodoma ikiwa ni katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani leo tarehe 5 Juni 2023. Amesema ni lazima kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wanaokiuka maagizo hayo pamoja na kuwataka watendaji wote wanaohusika kusimamia kwa karibu uzalishaji na matumizi ya mifuko mbadala.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba ni vema kuhakikisha mifuko yote inayozalishwa inaonesha taarifa za mzalishaji na kama inakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika. Pia amesisitiza makampuni na watu binafsi wanaozalisha bidhaa za plastiki kuhakikisha taka zinazotokana na bidhaa zinazozalishwa zinakusanywa na kuondolewa.
Halikadhalika Makamu wa Rais amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kampuni zinazopewa kazi ya kuzoa taka ziwe na uwezo kufanya kazi hizo kwa ufanisi. Amekemea utoaji wa tenda za uzoaji taka kwa kampuni zisizokuwa na uwezo na zile zisizo na vitendea kazi vya kisasa na kuzitaka Halmashauri kuweka miundombinu ya uhakika ya ukusanyaji na usombaji wa taka katika mitaa na maeneo ya mikusanyiko kama sokoni, stendi na hospitalini.
Aidha Dkt. Mpango ametoa wito kwa wananchi kutambua wajibu walionao katika kutunza vyanzo vya maji, kuacha mazoea ya kutupa taka hovyo na kuagiza kila kaya kuwa na sehemu mahsusi ya kuhifadhia ama kuchomea taka. Amesema masuala ya kufanya usafi na utunzaji mazingira hayana mbadala kwa kuwa mazingira ndio uhai na yana mahusiano ya moja kwa moja na ustawi wa Taifa kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira limeendelea kupewa kipaumbele hapa nchini ambapo kwa kutumia Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kauli mbiu iliopo ni yenye lengo la kuhamasisha ajenda ya utunzaji wa mazingira na kutunza vyanzo vya maji.
Dkt Jafo amewapongeza wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu kwa kujitoa kihifadhi mazingira ikiwemo kampeni ya soma na mti yenye lengo la kuhamasisha upandaji wa miti mashuleni. Halikadhalika amewashukuru wadau mbalimbali katika jitihada zao za kuhakikisha suala la mazingira linapewa kipaumbele kwa maendeleo endelevu.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema mkoa huo unaendelea na kampeni ya kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki ambapo tayari kwa kushirikiana na NEMC waliweza kukifungia kiwanda kimoja kinachozalisha mifuko hiyo. Amesema elimu inaendelea kutolewa katika masoko na maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanaachana na matumizi ya mifuko hiyo.
Pia ameongeza kwamba Mkoa huo utaendelea na jitihada za kulinda vyanzo vya maji ikiwemo chanzo cha maji Mzakwe kwa kusimamia na kupanda miti katika eneo hilo muhimu. Amesema mkoa utaendeleza hamasa ya usafi wa mazingira iliofanyika katika wiki ya kuadhimisha siku ya mazingira duniani hususani usafi katika mifereji ya jiji la Dodoma.
Zoezi la kufanya usafi katika soko kuu la wamachinga mjini Dodoma limewashirikisha viongozi mbalimbali, wananchi na watumiaji wa soko hilo. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2023 inasema “Shinda uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki”
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
05 Juni 2023
Dodoma.
Waheshimiwa Viongozi, Ndugu Wananchi na Wadau wa Mazingira, Kila mwaka ifikapo tarehe kama ya leo 05, Juni, Jumuiya ya Kimataifa huadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Hivyo, Tanzania pia kama sehemu ya Jumuiya, tunaungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha siku hii muhimu sana. Lengo kuu la maadhimisho haya ni kukumbushana juu ya wajibu wetu katika kuhifadhi, kulinda na kuendeleza jitihada za uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
Ndugu Wananchi na Wadau wa Mazingira,
Kaulimbiu ya siku hii ya Mazingira mwaka huu inasema, “Shinda uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki” (Beat Plastic Pollution). Kaulimbiu hii inaitaka Jumuiya ya Kimataifa, ambayo Tanzania pia ni sehemu yake, kuendelea kuweka juhudi za makusudi kupinga na kuondokana na matumizi ya bidhaa za plastiki ambazo zinachafua sana
mazingira duniani.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2019 wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa Makamu wa Rais, Serikali ilifanya uamuzi na Kampeni kubwa ya kusitisha matumizi ya mifuko ya plastiki nchi nzima na kuagiza itumike mifuko mbadala ambayo ni rafiki zaidi kwa mazingira yetu. Kampeni hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa, na Tanzania ilisifika kimataifa kuwa miongoni mwa nchi zilizofanikiwa kupunguza taka za plastiki. Lakini inasikitisha kuona kuwa, matumizi ya mifuko ya plastiki yameanza kurudi kwa kasi! Tunashuhudia katika maeneo yetu tunayoishi hususan katika mifereji ya maji, kando ya barabara na maeneo mengine ya wazi, kuongezeka kwa taka za plastiki.
Inakadiriwa kuwa, kila mwaka dunia inatumia mifuko bilioni 500 ya plastiki. Aidha, asilimia 10 ya taka tunazozalisha zinatokana na plastiki. Sehemu kubwa (80%) ya taka zinazoishia baharini na katika maziwa kupitia mito na mitaro ya maji ya mvua na upepo ni za plastiki. Hali hii inaathiri sana viumbe maji na pia inaharibu miundombinu ya barabara ikiwemo kuziba mifereji. Hapa nchini, takriban tani 350,000 ya mifuko ya plastiki huzalishwa kila mwaka na zaidi ya asilimia 70 ya taka katika Bahari ya Hindi ni zile zitokanazo na plastiki! Hali hii ikiachwa iendelee, kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa taka za plastiki nyingi zaidi katika bahari zetu kuliko samaki na viumbe hai vingine. Katika miaka michache ijayo wavuvi watakuwa wanavua maplastiki badala ya samaki. Sote tumeshashuhudia athari mbalimbali zitokanazo na taka za plastiki ambazo nimeshazisema. Kwa bahati mbaya sana, taka za plastiki haziozi haraka! Inakadiriwa kuwa mifuko ya plastiki huchukua miaka 400
mpaka 1000 kuoza. Ni wazi kuwa hatuwezi kuacha hali hii iendelee! Hivyo, nawasihi watanzania wote tuhakikishe kazi ya kudhibiti taka za plastiki inaendelezwa na kufanikiwa. Tuendelee kupiga vita kwa nguvu zote matumizi ya mifuko ya plastiki na kuimarisha utunzaji wa mazingira yetu hususan bahari, maziwa na mito kwa kuepuka uchafuzi unaotokana na taka za plastiki.
Nawaomba wote tukishirikiane katika hili.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi na Wadau wa Mazingira,
Kwa kuzingatia hali ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira ilivyo hivi sasa hapa nchini, napenda kusisitiza yafuatayo:
Jambo la Kwanza, kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki. Bado kuna ukiukwaji wa Sheria unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaozalisha au kuingiza mifuko ya plastiki kinyemela. Lakini pia kuna wafanyabisahara wa bidhaa za sokoni ambao wanatumia mifuko ya plastiki (aina ya “tubings”) kama vibebeo/vifungashio vya bidhaa. Hii inarudisha nyuma hatua kubwa iliyofikiwa tangu Serikali ilipotoa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki. Hivyo, natoa maelekezo kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kusimamia na kuongeza nguvu zaidi katika utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki. Hakikisheni mnachukua hatua za kisheria kwa wanaokiuka maagizo haya. Vilevile, watendaji wote wanaohusika, wasimamie
kwa karibu uzalishaji na matumizi ya mifuko mbadala. Vilevile, wahakikishe mifuko yote inayozalishwa inaonesha taarifa za mzalishaji (yaani anuani na wapi inazalishwa) na kama inakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.
Aidha, kwa makampuni na watu binafsi wanaozalisha bidhaa za plastiki, hakikisheni taka zinazotokana na bidhaa zinazozalishwa, zinakusanywa na kuondolewa (Extended Producer Responsibility).
Pia nichukue fursa hii kuwasihi Watanzania wenzangu kuacha mazoea ya kutupa taka hovyo. Siyo utaarabu kila mahali kufanya ni jalala la kutupa taka! Tujenge tabia ya kuyaweka mazingira yetu kuwa safi. Kwa wale walioko maeneo ya mijini ni vema kila kaya kuwa na sehemu mahsusi ya kuhifadhia ama kuchomea taka. Aidha, wamiliki wa mabasi na magari binafsi wawe na vyombo au vikapu vya kuweka taka katika magari yao ili abiria wasitupe chupa za plastiki na taka nyingine barabarani au majini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiongoza Viongozi na Wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma kufanya usafi katika Soko Kuu la Wamachinga mjini Dodoma ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo tarehe 05 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi na Wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kuongoza zoezi la kufanya usafi katika Soko Kuu la Wamachinga mjini Dodoma ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo tarehe 05 Juni 2023.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi na Wadau wa Mazingira,
Jambo la Pili kwa mujibu wa Kifungu cha 89 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288, Halmashauri zimepewa mamlaka ya kutunga sheria ndogo za Utunzaji wa Mazingira na Udhibiti wa Taka. Uzoefu unaonesha kuwa kila Halmashauri ina Sheria Ndogo za Utunzaji wa Mazingira na Udhibiti Taka. Hata hivyo, bado kuna tatizo la usimamizi na utekelezaji wa sheria hizo. Taka za Plastiki na taka nyingine zimeendelea kuzagaa katika Majiji, Miji na Halmashauri zetu licha kuwepo kwa Sheria ndogo zilizotungwa kukabiliana na changamoto hiyo na kuhakikisha miji yetu inakuwa safi. Hivyo, naziagiza Halmshauri zote, ziandae utaratibu wa kusimamia utekelezaji wa sheria ndogo mlizojitungia na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wote watakaokiuka sheria ndogo hizo. TAMISEMI zisimamieni ipasavyo Halmashauri kutekeleza majukumu yake. Usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu, hivyo Halmashauri ziandae utaratibu pia wa kuelimisha wananchi umuhimu wa utunzaji wa mazingira yetu. Kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake katika kuhakikisha hakuna mwananchi anayetupa taka hovyo na kuchafua mazingira yetu. Vilevile, naelekeza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kutimiza wajibu wake wa kisheria katika usimamizi wa mazingira yetu. Simamieni majukumu yenu kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.
Jambo la Tatu, nazikumbusha Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe kuwa Kampuni zinazopewa kazi ya kuzoa taka ziwe na uwezo kufanya kazi hizo kwa ufanisi. Zipo baadhi ya Kampuni zinashindwa kutekeleza majukumu waliyopewa ipasavyo kutokana na kuwa na uwezo mdogo. Yaani unakuta Kampuni iliyopewa tenda ya kukusanya taka, magari yenyewe wanayotumia ni takataka! Unakuta gari limebeba taka liko wazi na taka zinatoa harufu kali hali inayosababisha kero kwa wananchi. Watumiaji wa barabara ya Pugu nadhani wananielewa ninachokisema. Nazikumbusha Halmashauri zote: acheni kutoa tenda kwa Kampuni zisizokuwa na uwezo na zile zisizo na vitendea kazi vya kisasa! Aidha, wekeni miundombinu ya uhakika ya ukusanyaji na usombaji wa taka katika mitaa na maeneo ya mikusanyiko kama sokoni, stendi na hospitalini.
Jambo la Nne, taka zinaweza kuwa ni mali pale zinapotumika kama malighafi ya viwanda. Halmashauri zote zihakikishe kuwa zinaweka mifumo na mazingira wezeshi ya kuhamasisha viwanda vya urejelezaji wa taka. Aidha, natoa wito kwa sekta binafsi kuongeza jitihada katika ukusanyaji na urejelezaji wa taka hususan zile zitokanazo na plastiki.
Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta, kaeni na sekta binafsi kutafuta wawekezaji zaidi katika
teknolojia ya kubadili taka mbalimbali ili ziweze kutumika tena kama bidhaa, mfano kuwa nishati ama mbolea. Hatua hii itachochea ukuaji wa viwanda vya urejelezaji (recycling industries) na hivyo kuchangia katika uchumi wa nchi na ajira nchini.
Jambo la Tano, napenda kutumia fursa hii kuhimiza juu ya wajibu wetu wa kutunza vyanzo vya maji. Tusipozingatia wajibu huu, tutaiweka Nchi yetu katika hatari kubwa ya janga la ukosefu wa maji. Nawakumbusha kuwa wakati Serikali inatekeleza azma yake ya kusambaza maji safi na salama,
wajibu wa wananchi ni kuhakikisha kuwa tunahifadhi vyanzo vya maji. Tusipozingatia wajibu huu, uwekezaji mkubwa wa fedha za Serikali katika miundombinu ya miradi ya maji mijini na vijijini haitakuwa na maana yoyote kwa kuwa hakutakuwa na maji yatakayotiririka katka mabomba hayo. Aidha, ni muhimu utunzaji wa vyanzo vya maji uende sambamba na uhifadhi wa misitu yetu ambayo inatuwezesha kupata mvua na kutufanya tuweze kulima na kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula biashara.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi na Wadau wa Mazingira,
Masuala ya kufanya usafi na utunzaji mazingira hayana mbadala, kwa kuwa mazingira yetu ndio uhai wetu na ndio uchumi wetu. Ustawi wa mazingira una mahusiano ya moja kwa moja na ustawi wa Taifa kiuchumi na kijamii. Tukitunza mazingira yetu, tutakuwa tumeinua ustawi wa Taifa letu. Hivyo, napenda kuziagiza Halmashauri zote nchini, kuhakikisha kwamba suala la utunzaji na usafi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa taka za plastiki, linapewa kipaumbele katika mipango ya bajeti. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kulinda
mazingira yetu na kupunguza magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira. Aidha, hakikisheni mnaandaa mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu muhimu ili kuwa na mfumo bora wa kudhibiti taka katika Halmashauri zenu. Napenda pia kuwasihi wananchi wote kufanya usafi katika maeneo ya makazi yetu kila siku na kushirikiana na Serikali za mitaa kutunza na kuhifadhi mazingira kwa faida yetu sote. Napenda pia kuwashukuru wananchi na wadau wote mliojitokeza kushiriki katika kuadhimisha siku hii. Aidha, ninawasisitiza kuhakikisha kuwa miti mliyoipanda inatunzwa na kukua na zoezi la usafi na uhifadhi wa mazingira linakuwa endelevu.
Baada ya kusema hayo, sasa ninatamka rasmi kuwa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani hapa nchini yamefikia kilele.
Asanteni kwa kunisikiliza!