Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kundi linalojiita Ushirika wa Maendeleo ya Kongo, CODECO lenye wanamgambo wengi kutoka kabila la Lendu, wamekuwa wakishambulia mara kwa mara kambi za watu waliokimbia makazi yao huko Ituri.
Wanamgambo hao walishambulia nyakati za usiku kambi ya Lala , ambayo ilikuwa inawahifadhi wakimbizi wengi wa ndani kutoka kabila la Hema. Wapiganaji hao waliendesha mauaji hayo kwa kuwapiga risasi, kuwakata mapanga na kuwachoma moto watoto wapatao 23, wanawake 13 na wanaume 10 huku wengine 8 wakijeruhiwa. Wanajeshi wa Kongo pamoja na kikosi cha walinda amani cha Umoja wa Mataifa waliokuwa katika mji ulio karibu wa Bule hawakuingilia kati.
Thomas Fessy mtafiti mkuu anayehusika na Kongo katika shirika la Human Rights Watch anasema imekuwa jambo la kawaida kwa kundi la CODECO kushambulia raia katika kambi wanazotafuta kimbilio kutokana na ghasia, licha ya kuwa kambi hizo zinapaswa kuwa maeneo salama badala ya maeneo ya mauaji.
Pia anasema kuwa ni muhimu kwa Jeshi la Kongo na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu lao la ulinzi ili kuhakikisha kuwa watu waliokimbia makazi yao wanakuwa salama.
Matukio ya sasa ya ghasia na kulipiza visasi yanayojirudia huko Ituri, ambayo yalianza Desemba mwaka 2017, yanatokana na masuala ya muda mrefu ambayo hayajashughulikiwa tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, wakati makumi kwa maelfu ya raia walikufa katika mauaji ya miaka 1999 hadi 2007.
Migogoro iliyorithiwa kutokana na ukosefu wa usawa wakati wa enzi za ukoloni kama vile haki za umiliki wa ardhi, mahusiano ya kikabila, uingiliaji wa masuala ya kikanda na udhibiti wa maliasili kati ya jamii hasa zile za Wahema na Lendu inaonekana kuwa kiini cha matatizo hayo.
Wakati mauaji hayo ya kinyama yakiendelea, wakimbizi na wakaazi wa kijiji jirani cha Lodinga, walipiga simu na kutoa tahadhari kwa wanajeshi wa Kongo na vikosi vya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Kongo, MONUSCO lakini hawakupata msaada wowote.
Human Rights Watch ilizungumza kwa njia ya simu na manusura tisa pamoja na mashahidi wengine ambao walisema waliamshwa na milio ya risasi wakati wapiganaji wakiishambulia kambi hiyo.
Wanajeshi wa Kongo walikuwa katika kituo chenye umbali wa kilomita 1.5 lakini waliwasili kambini hapo baada ya jua kuchomoza na wanamgambo kuondoka na walisaidia kukusanya maiti na kuhakiki waliojeruhiwa. Nao askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walikuwa umbali wa kilomita sita katika kambi moja huko Bule hivyo wakashindwa kufika pia.
Afisa mkuu wa Ujumbe huo, Meja Imran Tareq anasema walishindwa kufika eneo la tukio kutokana na kifaru kimoja kuharibika na hivyo kushindwa kutimiza sharti la kuwa na msafara wa magari mawili kama inavyoagiza kanuni wakati wa operesheni kama hizo.
Hata hivyo, idara ya Operesheni za kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa inasema kwamba MONUSCO inafanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo, na iwapo uchunguzi utabaini kuwa wanajeshi hao hawakutimiza wajibu wao bila sababu zozote za msingi, basi watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
#monusco
#humanrightswatch
#KonceptTvUpdates