Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji nchini (EWURA) imepokea taarifa ya uwepo wa baadhi ya Kampuni za Mafuta KUHODHI mafuta kwa ajili ya maslahi binafsi ya kibiashara ikiwemo kusubiri mabadiliko ya bei, jambo ambalo ni ukiukwaji wa utaratibu wa biashara.
Aidha, kampuni nyingine zimeripotiwa kupakia mafuta kutoka kwenye maghala pasipo kuyauza na nyingine kukataa kuuza mafuta kwa wamiliki wa vituo wasio kuwa na ubia au mikataba nao. Kutokana hali hiyo, EWURA imepata taarifa ya kuchelewa kufikishwa kwa mafuta katika baadhi ya maeneo ya pembezoni mwa nchi na Miji.
EWURA imependa kuwajulisha wananchi wote kuwa nchi ina mafuta ya kutosha katika maghala ya kuhifadhia mafuta na wakati huo huo meli zenye shehena ya mafuta kutoka nje ya nchi zinaendelea kuingia na kushusha mafuta kama kawaida chini ya uratibu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).
Mpaka tarehe 14 Julai 2023 mafuta yote yaliyokuwepo nchini ni lita 169,853,692 za mafuta ya petroli, lita 209,641,670 za diezeli na lita 34,588,002 za mafuta ya ndege yanayotoshelea mahitaji.
Kulingana na taarifa hizo, EWURA inatoa ONYO kwa kampuni za mafuta zinazohodhi mafuta na kuzitaka kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, kanuni zinazosimamia biashara ya mafuta ya petroli nchini na masharti ya leseni zao za biashara.
KonceptTvUpdates