Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Dkt. Charles Msonde amewapongeza Walimu na Viongozi wa Elimu Mkoa wa Singida kwa kusimamia na kutekeleza kikamilifu vigezo vya kuboresha elimu nchini (KPI).
Ametoa Pongezi hizo wakati akitembelea na kukagua miradi ya maendeleo pamoja na utoaji wa elimu kwenye shule za msingi na sekondari katika halmashauri zote za mkoa wa Singida.
“Wanafunzi waliyo yaonesha hapa katika shule ya Sekondari Tumaini na Lukumba zilizopo Iramba vilevile niliyoyaona katika shule ya Msingi Ikungi, yamedhibitisha pasipo shaka, kwamba Walimu mnatekeleza na ni waumini wa kutekeleza Vigezo vya kuboresha elimu Tanzania (KPI)” amesisitiza Msonde
Dkt. Msonde amesema lengo la Serikali la Kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari ni kuhakikisha Mazingira ya Wanafunzi ya kujifunza na Mazingira ya Walimu ya kufundishia yakuwa bora ili Watoto wapate ujuzi, umahiri na malezi bora.
Aidha, Ameeleza kuwa dira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona wanafunzi wote wanapata ujuzi na umahiri kwa kila ngazi wanayopitia ambapo wenye jukumu la kumsaidia katika Utekelezaji wa jambo hilo ni Walimu.
“Ukombozi wa elimu katika nchi yetu ya Tanzania unaletwa na walimu ndio maana tukaamua kuimarisha vigezo vya ufundishaji ili kila mwalimu anapofundisha ahakikishe kila mwanafunzi anakuwa na uelewa katika somo kila analofundishwa”