Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wamezuru jamii ya Wahadzabe wanaoishi katika kijiji cha Endamagha kilichopo tarafa ya Eyasi, wilaya ya Karatu, ambapo Dkt. Kikwete alitumia fursa hiyo kuwapongeza wenyeji wake kwa kuendelea kudumisha mila na desturi zao huku wakitambua na kuzingatia umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shule ili kupata elimu itakayokuja kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye.
“Katika ziara hii hapa kwenye kijiji cha Endamagha wilayani Karatu mimi na mke wangu tumepata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ya mila na desturi za jamii ya Wahadzabe hususani njia zao za asili za kutafuta na kuhifadhi vyakula, malezi ya watoto, makazi yao,lakini pia changamoto zinazowakabili kama vile upatikanaji wa elimu kutokana na mfumo wao wa maisha wa kuhamahama, uvamizi wa makabila mengine katika maeneo yao ya asili na upatikanaji wa huduma nyingine muhimu za kijamii” Dkt. Jakaya Kikwete. Rais Mstaafu