
Kupitia hotuba aliyoitoa kwa taifa lake siku ya jana Rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa amesema nchi hiyo haipo kwenye shinikizo la kuegemea upande wowote wa mataifa yenye nguvu Zaidi duniani ama makundi ya mataifa yenye ushawishi kwani taifa hilo halivutiwi na ushindani wowote kutoka kwa mataifa yenye nguvu.
Hayo yanajiri mara baada ya Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa maandalizi ya mkutano wa kilele cha mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani yaani BRICS ambapo jumiya hiyo inaundwa na Brasil, Urusi, India, China Pamoja na nchi mwenyeji Afrika Kusini.
Ikumbukwe kuwa taifa hilo la Afrika Kusini limekataa kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mzozo ambao umedumu kwa miezi 18 mpaka hivi tangu kutokea kwake mwezi Februari mwaka wa 2022 ambapo mataifa mengi duniani yataangazia Zaidi uhusiano wa Afrika kusini na Urusi kwenye mkutano huo.
Mkutano huo utahudhuriwa na rais wa china xi jinping, rais wa Brasil Luis Inacio Lula da Silva, Waziri mkuu wa India Narendra Modi huku Urusi ikimkosa Rais wake Vladimir Putin ambaye atashiriki kupitia mtandao mara baada ya kuandamwa na waraka wa kukamatwa uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC ambapo Afrika kusini inapaswa kutekeleza hilo hivyo Urusi itawakilishwa ana kwa ana na Waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov.
Akizungumzia uhusiano huo wa mataifa ya BRICS, Siyabonga Cyprian Cwele, balozi wa Afrika Kusini nchini China amesema kuwa BRICS sio kundi na hawashindani na makundi mengine yoyote ya kimataifa. Cwele ameongeza kuwa BRICS ni ushirikiano wa maendeleo na ingawa vyombo vya habari vinaweza kujaribu kuwatenganisha, wanaheshimiana sana kwa sababu wanajua kinachowaunganisha.
Wakati wa mkutano huo wa kilele ukitarajiwa, Urusi na China zitakuwa zinasaka kunufaika zaidi kisiasa na kiuchumi katika mataifa yanaoyoendelea. Licha ya Malalamiko ya pamoja dhidi ya mataifa ya Magharibi kutoka kwa mataifa hayo yanayoendelea huenda yakachukuwa mwelekeo mkali zaidi kwa kuileta karibu Saudi Arabia.
Mkutano huo wa kilele wa siku ya Jumatano na mikutano ya pembezoni siku ya Jumanne na Alhamisi, inatarajiwa kutoa miito ya jumla ya ushirikiano zaidi miongoni mwa mataifa ya Kusini huku kukiwa na ongezeko la kutoridhika kuhusu dhana ya uongozi wa mataifa ya Magharibi katika taasisi za kimataifa
#KonceptTVUpdates