Jeshi la polisi mkoa wa Morogoro linamsaka Harid Njianguru mkazi wa Kidatu Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kwa tuhuma za kumshambulia mteja wake na kusababishia madhara makubwa baada ya kushindwa kulipa kiingilio cha Sh 500 kuangalia mpira kati ya timu ya soka ya Azam FC na Tanzania Prisons kwenye ukumbi wa baa anayomiliki.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa morogoro, Alex Mkama na kusema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa Agosti 28, 2023 katika kijiji cha Mkamba Wilaya ya Kilombero baada ya mfanyabiashara huyo kumshambulia Protas Komba (40) kwa kumpiga na kisha kumsukuma na kuangukia kisogo na kupoteza fahamu.
Kamanda Mkama amesema Komba alifika baa ya mfanyabiashara huyo ambayo inajulikana kwa jina la‘Kigamboni’ ili kuangalia mchezo huo na kwamba alishindwa kulipa kiingilio cha sh 500 na akawa analazimisha kuingia ndani ya baa.
Kamanda Mkama amewaomba wananchi kuwa popote mtuhumiwa huyo atakapoonekana watoe taarifa zake ili aweze kukamatwa kwa sababu hawezi kuwa salama kwa namna yoyote ile.
Mkama alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watumie njia zinazokubalika kisheria na kupata haki zao.
“Michezo ni burudani na kama mtu anatafuta burudani basi ifanyike namna ya kuweza kufanya mazugumzo kama kuna ulazima ili na yeye aweze kushiriki kwenye burudani, kama haiwezekani basi atumie lugha za staha kuliko mkumzuia na kusababisha kitendo kilichofanyika kilicholeta madhara makubwa.” alisema Mkama
#KonceptTVUpdates