Uongozi wa Klabu ya timu ya mpira wa miguu AZAM FC Agosti 30, 2023 katika Kituo cha Polisi Mbande imekabidhi samani za ofisi kwa ajili ya kufanikisha ufanisi na utendaji kazi wa Polisi kwa lengo lakuisaidia jamii.
Mkuu wa Idara ya habari wa Klabu hiyo Zaka Thabiti amekabidhi meza nne na viti vinne vyenye thamani ya Tshs. 5,000,000 Milioni tano kwa ajili ya Kituo hicho.
Zaka amesema kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likitoa mchango mkubwa kwa jamii katika kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaimarika.
Ameeleza kuwa uhusiano wao na Jeshi la Polisi ni endelevu kwa vile wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi katika kusimamia ulinzi wa michezo mbalimbali inayofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi na ameahidi kuendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri kati ya Klabu hiyo na Jeshi la Polisi.
ACP Kungu Malulu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke ameishukuru Klabu hiyo kwa kuthamini juhudi za Jeshi la Polisi na kutoa Samani za ofisi zitakazosaidia Askari kufanya kazi kwa weledi na kuihudumia jamii.
Amesema vifaa hivyo vimefika muda sahihi kwa vile kituo hicho kinaelekea kufunguliwa rasmi tarehe 01/09/2023 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar Es Salaam SACP Jumanne Mulilo.
#KonceptTVUpdates