Huko Nachingwea, tarehe 31 Agosti 2023 – Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea limefanya kikao cha kisheria kwa mujibu wa kifungu Na. 43 cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa sura 290 (The Local Government Finance Act), pamoja na agizo katika kanuni za fedha za Serikali za Mitaa Na. 31 (The Local Authority Financial Memorandum of 2009). Kikao hiki, kilichoongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Adinani Mpyagila, na Katibu wake kaimu Mkurugenzi Ndugu Lington Nzunda, kilikuwa na lengo la kupitia taarifa za ufungaji wa hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023.
Kwa mujibu wa taratibu, Halmashauri zote zinatakiwa kuandaa taarifa za mwisho wa mwaka (Annual Statements) na kuziwasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kabla au ifikapo tarehe 30 Septemba ya kila mwaka. Baraza limepitia taarifa kuu tatu zinazojumishwa kwenye taarifa za hesabu za mwisho wa mwaka:
1. Mizani: Hadi kufikia Juni 30, 2023, Halmashauri ilikuwa na Mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 55.718.
2. Taarifa ya Mapato na Matumizi: Halmashauri ilipokea jumla ya Shilingi Bilioni 35.702 kutoka katika vyanzo mbalimbali. Mapato yaliongezeka kwa Shilingi Bilioni 3.459 na matumizi yalikuwa Shilingi Bilioni 29.317 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023.
3. Taarifa ya Mtiririko wa Fedha Taslimu: Jumla ya Shilingi Bilioni 35.542 zilionekana kupokelewa kutoka katika vyanzo mbalimbali. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 29.546 zilitumika katika shughuli za kawaida na Shilingi Bilioni 1.913 zilitumika katika shughuli za uwekezaji. Mwisho wa mwaka wa fedha, Halmashauri ilibakiwa na jumla ya fedha Shilingi Bilioni 4.083 kwenye akaunti mbalimbali.
Baada ya kupitia taarifa hizi, Waheshimiwa Madiwani wameridhishwa na kusifia matumizi sahihi ya fedha za Halmashauri. Hii ni hatua muhimu kuelekea uwazi na uwajibikaji katika utumiaji wa raslimali za umma.
#KonceptTvUpdates