WAKURUGENZI wa Halmashauri tano ambao hawakutimiza mpango wa utengaji fedha za kutekeleza afua za lishe kulingana na idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano watakiwa kuhakikisha wanatenga fedha hizo kabla ya Desemba mwaka huu.
Maagizo hayo yametolewa leo Agosti 29,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki wakati wa kufungua mkutano wa mwaka wa tathimini ya saba ya Utekelezaji wa mkataba wa lishe Nchini.
Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri tano za Mpanda DC, Kasulu DC, Mkalama DC, Uyui DC na Lushoto DC ambazo katika mipango yao hawakuzingatia kiasi cha fedha kulingana na idadi ya Watoto chini ya miaka mitano watekeleze maelekezo yaliyotolewa ifikapo Desemba, 2023 wakati wa kufanya mapitio ya bajeti.
Mhe.Kairuki ametoa rai kwa wakuu wa Mikoa kusimamia Halmashauri zao kwa kuhakikisha fedha iliyopangwa kutekeleza afua za lishe zinatolewa kwa wakati.
“Hii inatokana na matokeo niliyo nayo ambayo inaonekana kuwa kiashiria hiki bado hakitekelezwi ipasavyo katika maeneo mengi. Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe kuwa fedha zinazotolewa zinaenda kutekeleza shughuli zilizopangwa na sio vinginevyo.” amesisitiza Mhe Kairuki
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa Wataalamu wa afya kulipa uzito unaostahili suala la lishe ili wananchi waone umuhimu wake katika kuchangia mapambano dhidi ya magonjwa na kuleta tija katika maendeleo kwa mtu binafsi na kwa taifa kwa ujumla.
“Ili tuwapunguzie viongozi wajao kazi ni lazima tuwekeze nguvu ya kutosha kwenye eneo la lishe.” Amesema Dkt. Mollel.
Ameendelea kusisitiza lishe sio suala la wajawazito peke yake na watoto, bali hata makundi mengine ni muhimu kupata lishe bora itayosaidia kutunza afya na kuongeza miaka mingi zaidi ya kuishi.
#KonceptTVUpdates