Maafisa wa jeshi walionyakua mamlaka katika mapinduzi nchini Gabon siku ya Jumatano wamemtaja Jenerali Brice Oligui Nguema kuwa kiongozi wa mpito wa taifa hilo la Afrika Magharibi.
Brice Nguema, kulingana na ripoti za vyombo vya habari ni binamu wa rais aliyeondolewa madarakani Ali Bongo.
Msemaji wa linalojulikana kama baraza la mpito, kupitia shirika la habari la serikali la Gabon 24, alimtangaza Nguema kama rais wa mpito jana jioni.
Saa chache baada ya viongozi wa kijeshi kutwaa mamlaka, Rais Ali Bongo alionekana kwenye ukanda wa video akitoa wito wa usaidizi.
Bongo amewataka raia wa Gabon “kupiga kelele” na kueleza kuwa amezuiliwa kinyume cha sheria katika maakazi yake.
Kundi la maafisa wa ngazi ya juu jeshini wameiambia televisheni ya taifa kuwa Bongo anatuhumiwa kwa uhaini mkubwa.
Wakati hayo yanaarifiwa, mashirika ya kikanda na kimataifa yameonyesha wasiwasi wao juu ya kinachoendelea huko Gabon.
#KonceptTVUpdates