Jukwaa la Katiba na Sheria Tanzania (JUKATA) limetoa ombi la kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan ili kujadili kwa kina kuhusu hali ya demokrasia nchini na hatua anazozichukua Rais katika kusimamia misingi ya R4: reconciliation, resilience, reforms, na rebuilding. Katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wadau mbalimbali wa haki za binadamu wameshauri kwamba ingawa Rais Samia ana dhamira njema ya kuimarisha demokrasia nchini, bado kuna changamoto ya baadhi ya watendaji kuzuia kufikia malengo hayo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa JUKATA, Ananilea Nkya, alieleza kuwa Rais Samia amedhihirisha dhamira yake ya kweli katika kusimamia misingi ya R4 ambayo inalenga kujenga umoja, kusameheana, kustahimiliana, kuleta mageuzi, na kujenga taifa imara pamoja. Hata hivyo, aliongeza kuwa kuna baadhi ya watendaji wanawakosesha Rais mwelekeo sahihi, wanachochea hisia mbaya dhidi yake na hivyo kuhatarisha juhudi zake za kuleta umoja na maendeleo.
Nkya alisema, “Kuna wale wanaomshauri vibaya Rais, wanamdhalilisha Rais kwa kutoa matamko yasiyo na tija na kusababisha hali ya wasiwasi katika taifa letu. Wanaweza kuonekana kama wanamsaidia Rais, lakini kwa kweli wanachangia kujenga chuki kati yake na wananchi. Wanapaswa kumsaidia Rais badala ya kumtia katika machafuko.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, alisoma taarifa ya pamoja iliyotolewa na wadau hao wa haki za binadamu. Taarifa hiyo iliiomba Jeshi la Polisi kuwaachia huru watu wote wanaodaiwa kukamatwa kutokana na kukosoa mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA). Watu hao ni pamoja na Dk Willbroad Slaa, Peter Madeleke, Boniphace Mwabukusi, na Mdude Nyagali.
Wadau hao, wakiwemo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), walisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki na uhuru wa kutoa maoni. Pia, walitoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua ili watuhumiwa waachiwe bila masharti yoyote.
Henga alisema, “Tunamwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati suala hili ili watuhumiwa waachiwe bila ya kizuizi chochote. Pia, tunataka Jeshi la Polisi kuheshimu haki na uhuru wa kutoa maoni kulingana na mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande kuhusu mfumo wa haki jinai nchini.”
Katika kipindi hiki cha mageuzi na kujenga taifa imara, ushirikiano na majadiliano yenye tija ni muhimu katika kuendeleza demokrasia na haki za binadamu. Wadau wa haki za binadamu wanasema wanaimarisha juhudi zao ili kuhakikisha kuwa mchakato wa kuleta mageuzi na mabadiliko nchini unafanyika kwa uwazi, usawa, na kwa kuzingatia haki za kila mwananchi.
#KonceptTvUpdates