Wananchi wa tarafa ya Naipanga, wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi wamelalamika kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa maji safi na salama. Ingawa wamekuwa wakilalamika mara kadhaa kuhusu suala hili, serikali imeshindwa kutatua tatizo hilo.
Wakizungumza katika mkutano na uongozi wa Wilaya ya Nachingwea, katika Kata ya Chiumbati Shuleni, Kijiji cha Chiwindi, wananchi wamesema suala la maji limekuwa kero kubwa kijijini hapo. Wanapoteza muda mwingi kutafuta maji na hali hiyo inawaathiri kwa kuacha shughuli zingine, ikiwa ni pamoja na shule na nyumba za ibada.
Kila kijiji katika Tarafa ya Naipanga, kuna kirula kimoja kilichojengwa na Mamlaka ya Maji wilayani Nachingwea, lakini kirula hicho hakitoshi na maji hupatikana kwa nadra. Wananchi wamelalamika kuwa maji hukatika kwa muda mrefu bila taarifa ya ubovu ama matengenezo.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi – Nachingwea (Manawasa) kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kutoa taarifa ya ubovu au marekebisho.
Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini wanakiri kuifahamu kadhia hiyo ya maji katika Tarafa ya Naipanga, lakini bado changamoto kubwa ni kukosekana kwa vyanzo vya maji kijijini hapo. Serikali inahitajika kufanya juhudi zaidi ili kutatua tatizo hili la maji.
#KonceptTvUpdates
#Nachingwea