Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amesifu hatua ya Rais Samia kukaa kimya dhidi ya kauli zinazotolewa kupinga mkataba huo. Ameeleza ni imani yake kuwa, ukimya huo hauna maana ya kutofanyia kazi kinachopendekezwa, bali inahitajika hekima ya kuliendea jambo hilo na kwamba muafaka utapatikana.
Ameyasema hayo jijini Arusha Jumatatu Agosti 21, 2023 wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya kuanzishwa kwake mwaka 1963 baada ya muungano wa makanisa saba ya Kilutheri Tanzania.
Katika hotuba yake hiyo, Askofu Shoo ameeleza uwepo wa hali inayokaribia kuligawa taifa, wengine wakitumia sababu za kidini, wapo wenye maslahi yao ya kisiasa na yale ya kiuchumi.
“Nashukuru Mungu amekujaalia hekima kama mama na kiongozi umekaa kimya lakini kimya chako hicho sio kwamba hufanyii kazi, mimi nasema jambo hili linahitaji hekima kubwa ya kuliendelea na sisi tunakuombea kwa Mungu ili heshima yote itumike ili kuliendea jambo hili ili muafaka upatikane,” amesema Askofu Frederick Shoo.
Kauli hiyo ya Askofu Dk. Shoo inakuja wakati ambapo Kanisa Katoliki lenye waumini wengi zaidi nchini Tanzania, kutoa waraka wa kupinga mkataba huo wa bandari, ambao hapo jana Jumapili ulisomwa kwenye makanisa yote.
Ingawa katika hotuba yake, Askofu Dk. Shoo hakuutaja moja kwa moja waraka huo wa Kanisa Katoliki, lakini ameonekana kupingana nao, na kumtaka Rais Samia kuwa mvumilivu na mwenye busara katika kushughulikia maoni ya watu kuhusu mkataba huo wa Bandari.
Rais Samia aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amepongeza ushirikiano miongoni mwa taasisi za dini na serikali ya Tanzania na kuahidi kuuendeleza na kuwa tayari kushauriana na viongozi wa dini na madhehebu zote.