Kwa mujibu wa katiba ya nchi, Novemba 2024, Marekani itashuhudia uchaguzi wake wa urais wa 60, na kwa sasa, chama cha Republican kinajipanga kwa kufanya mdahalo wa wazi kuchagua mgombea wake. Katika mdahalo wa hivi karibuni uliofanyika Marekani, mgombea Vivek Ramaswamy ameibua mjadala mkubwa kwa kutangaza msimamo wake wa kutounga mkono msaada kwa Ukraine.
Mdahalo huo wa wagombea nane wa Republican ulifanyika siku ya Alhamisi, Agosti 24, 2023, na ulikuwa na mjadala mkubwa juu ya sera za kigeni na jinsi Marekani inavyopaswa kushughulikia uhusiano wake na nchi nyingine. Hata hivyo, kivutio kikubwa cha mdahalo huo kilikuwa kauli ya Vivek Ramaswamy kuhusu Ukraine.
Ramaswamy, mgombea mwenye msimamo mkali, aliweka wazi kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani, hatoitenga nchi hiyo ya Ulaya ya Mashariki kwa msaada wa ziada, hususan katika mgogoro wake na Russia. Aliita hatua hii “kupoteza rasilimali za nchi,” akisisitiza kuwa rasilimali hizo zinapaswa kutumika ndani ya Marekani.
Katika kutoa hoja yake, Ramaswamy alikashifu serikali ya sasa na kuzikosoa ziara za viongozi wastaafu wa Marekani, Mike Pence na Chris Christie, nchini Ukraine. Alihoji kuwa msaada wa Marekani kwa Ukraine ni “hasara kubwa” na kwamba rasilimali za kijeshi zinazopelekwa Kyiv zinaweza kutumika kwa manufaa ya Marekani yenyewe.
“Hii ni janga, tunalinda mipaka ya mtu mwingine wakati tunapaswa kutumia rasilimali hizo kuzuia uvamizi kwenye mipaka yetu,” alisisitiza Ramaswamy.
Hata hivyo, kauli hii ya Ramaswamy ilipingwa vikali na mwanadiplomasia na mwanachama mwenzake wa chama, Nikki Haley, aliyemuita Ramaswamy kuwa mtu asiye na uzoefu wa kutosha katika masuala ya diplomasia.
“Inaonesha huna uzoefu katika sera za kigeni,” alijibu Nikki.
Mdahalo huo wa Republican ulikuwa na mgawanyiko mkubwa wa maoni juu ya sera za kigeni na jinsi Marekani inavyopaswa kuelekeza rasilimali zake za kijeshi na kiuchumi. Wagombea wengine waliohudhuria mdahalo huo ni pamoja na Ron DeSantis, Mike Pence, Chris Christie, Tim Scott, Asa Hutchinson, na Doug Burgum.
Uamuzi wa Ramaswamy wa kutounga mkono msaada kwa Ukraine unaweza kuwa na athari kubwa kwa mkondo wa sera za kigeni za Marekani ikiwa atapata uungwaji mkono wa kutosha kutoka kwa wapiga kura wa Republican. Hata hivyo, mdahalo huo umezua maswali muhimu juu ya jinsi Marekani inavyopaswa kuendeleza uhusiano wake na nchi washirika, na jinsi rasilimali zinavyopaswa kutumika katika siasa za kimataifa.
Ni wazi kuwa mjadala huu utaendelea kuwa kivutio kikubwa katika kampeni za uchaguzi wa 2024 na kuweka msingi wa sera za nchi hiyo katika miaka ijayo.
#KonceptTvUpdates