Kampuni ya META, inayomiliki mitandao maarufu kama vile Facebook, Instagram, WhatsApp, na Threads imefanya tangazo kubwa. Mwanzilishi wa kampuni hiyo, Mark Zuckerberg, amethibitisha kuwa Threads itapata maboresho makubwa kwenye “Application” yake. Hatua hii inalenga kuongeza uwezo na urahisi wa matumizi kwa watumiaji wa mtandao huu.
Watumiaji wa mtandao wa Threads wanaweza kufurahia maboresho kadhaa yanayotarajiwa kuanza kutumika wiki hii. Moja ya maboresho hayo ni uwezo wa kuandika maneno kwenye picha au video wanazochapisha, kama inavyofanyika kwenye jukwaa la TikTok. Hii inawapa watumiaji fursa ya kuleta ubunifu wa ziada kwenye machapisho yao.
Vilevile, Threads itapata uwezo wa kumtaja au kum-mention mtu mwingine kwenye chapisho lako. Kwa mfano, unaweza kutaja jina la mtu kwenye chapisho lako, kama njia ya kuwaelekeza au kuwashirikisha katika mazungumzo yako.
Sehemu nyingine ya maboresho haya ni uwezo wa kushiriki chapisho (post) kutoka Threads moja kwa moja kwa mtu mwingine kupitia Instagram Direct Message (DM). Hii inafungua njia mpya ya kushirikiana na kubadilishana yaliyomo kati ya majukwaa haya mawili maarufu.
Hatua nyingine kubwa ni ujio wa toleo la mtandao wa Threads kwenye kompyuta. Hii inamaanisha kuwa watumiaji watapata fursa ya kuingia kwenye akaunti zao za Threads kupitia kompyuta kama ilivyo kwa mitandao mingine kama vile Instagram. Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha urahisi wa matumizi na kuwawezesha watumiaji kutumia mtandao huo kwa njia mbalimbali.
Hatua hizi za kuboresha Threads zinaonyesha dhamira ya kampuni ya META katika kutoa uzoefu bora kwa watumiaji wake. Maboresho haya yanatarajiwa kuleta athari chanya kwa watumiaji wa mtandao wa Threads, na kufanya jukwaa hilo kuwa mahali pa kuvutia zaidi kwa kushirikiana, kubadilishana mawazo, na kujenga jamii bora.
#EastAfricaTv
#KonceptTvUpdates