Baraza la Madiwani, Halmshauri ya Siha, mkoani Kilimanjaro, limeomba halmashauri hiyo kuwa taarifa mbali mbali zinazoletwa kwenye baraza hilo ziwasilishwe kwa lugha ya Kiswahili, ili wajumbe waweze kuchangia kwa mapana yake bila kukwama.
Hiyo ni mara baada Diwani wa Viti Maalumu, Lilian Mollel, kutaka kufahamu ni lini taarifa zinazokwenda kwenye baraza hilo, zitapelekwa kwa lugha ya Kiswahili, ili kila mjumbe wa baraza hilo, aweze kuchangia bila kukwama kutokana na kutokuwa na uelewa wa lugha inayotumika.
Wakizungumza kwenye baraza hilo maalumu ambalo linajadili ufungaji wa hesabu za halmshauri kwa mwaka 2022 na 2023, wamesema ni muhimu taarifa kuwa katika lugha ya Kiswahili ambayo madiwani wengi wanauelewa nayo na kimsingi ndiyo wanaendeshea vikao vyao.
Wamesema Serikali kila siku inapigia debe kuhusu kukua kwa lugha ya kiswahili duniani na kwamba baadhi ya nchi wameaanza kufundisha lugha hiyo, hivyo wanadhani siyo jambo jema kwa taarifa kuendelea kupelekwa katika baraza hilo zikiwa zimeandikwa kwa kiingereza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmshauri hiyo, Dancani Urasa, amesema: “Nafikiri taarifa zije kwa mfumo wa lugha ya kiswahili, hata kipindi cha nyuma tulishasema taarifa zije kwa lugha hiyo ya Kiswahili, hii inarahisisha kazi.”
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri hiyo, Naomi Swai amesema jambo hilo litfanyiwa kazi.
“Mawasiliano ni pale ambapo anayetoa taarifa na anayepokea taarifa wanaelewana, na sasa nchi yetu na nchi nyingine Duniani, kiswahili kinashika kasi sana, na sisi lazima tuendelee kukikuza na kukitangaza,” amesema Naomi.
#KonceptTVUpdates