Katika mji mkuu wa Niger, Niamey, mamia ya wafuasi wa mapinduzi walikusanyika katika mkutano siku ya Jumapili ili kuonyesha uungwaji wao mkono kwa utawala wa kijeshi.
Waandamanaji hao, waliokuwa wakipeperusha bendera za Niger na Urusi, walionesha mshikamano wao na wanajeshi waliomwondoa rais aliyechaguliwa, Mohamed Bazoum, mwezi uliopita.
Hii ilifuatia tangazo lililotolewa siku ya Jumamosi na kiongozi wa kijeshi, Jenerali Abdourahamane Tchiani, ambaye aliwaonya dhidi ya kuingiliwa kwa njia yoyote kutoka nje.
Aidha, alitangaza mpango wa kipindi cha mpito cha miaka mitatu, na kusema misingi ya mpito huo itaamuliwa ndani ya siku 30 katika “majadiliano” yatakayoandaliwa na viongozi wa mapinduzi.
Katika hotuba yake iliyotangazwa moja kwa moja baada ya kukutana na ujumbe wa amani kutoka kwa jumuiya ya kieneo ya Afrika Magharibi, Ecowas, Jenerali Tchiani alisema nchi hiyo haipendi vita lakini aliwaonya dhidi ya kuingiliwa kutoka nje.
Aliulaani vikali vikwazo vya Ecowas vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo na kusema kwamba vilikuwa havilengi kutafuta suluhisho bali “kutulemaza na kutudhalilisha”.
Hii ilikuwa ishara nyingine ya kutotii baada ya wapatanishi wa Ecowas kufanya mazungumzo ya amani na viongozi wa mapinduzi katika juhudi za mwisho za kufikia suluhisho la kidiplomasia kwa mzozo wa kisiasa.
Ecowas imeeleza kuwa kikosi chake cha dharura kiko tayari kuingilia kati ikiwa juhudi za amani za kutatua mzozo huo hazitafanikiwa.
#KonceptTvUpdates
#BBCSwahili