Baada ya kusikika malalamiko kadhaa mitandaoni kuhusu udahili wa wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu wakati huu dirisha la udahili limefunguliwa, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imejitokeza kutoa ufafanuzi muhimu kuhusu suala hili.
Moja ya malalamiko yanayojitokeza ni wanafunzi kukwama katika kufanya maamuzi ya vyuo vikuu wanavyotaka kuhudhuria. Imeelezwa kuwa kuna wanafunzi wanaopata nafasi katika vyuo kadhaa na hivyo wanakumbwa na changamoto ya kuona majina yao yamethibitishwa kwenye vyuo bila ridhaa yao.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa ametoa ufafanuzi kuhusu suala hili, akisema kuwa kuna changamoto za ujumla hasa kwa waombaji wapya wanapotumia mfumo wa kufanya maombi. Wanafunzi wengine hushindwa kutumia vizuri mfumo huu, na hivyo, amewataka vyuo kutoa elimu kwa wanafunzi na watumiaji wa mtandao wa maombi ili kusaidia kupunguza changamoto hizo.
Profesa Kihampa pia amesisitiza kwamba hakuna mwanafunzi atakayenyimwa fursa ya kusoma kwenye chuo anachokitaka iwapo amefikisha vigezo vinavyohitajika. Amewahimiza waombaji ambao wanakumbwa na changamoto kufika TCU kwa msaada na ufafanuzi zaidi.
Aidha, TCU imefahamisha kuwa kuna hawamu tatu za kufanya udahili na hata inapobidi, wataongeza madirisha ya udahili ili kushughulikia changamoto zozote zitakazojitokeza katika mchakato huu muhimu wa kujiunga na vyuo vikuu.
Hivyo basi, kwa ufafanuzi huo kutoka TCU, inatarajiwa kuwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu wataweza kupata mwongozo na msaada wa kutosha ili kufanikisha safari yao ya elimu ya juu bila vikwazo visivyo vya lazima.
#KonceptTvUpdates