Katika kona za mitaa na mikoa mbalimbali nchini Tanzania, kuna muziki ambao umekua kwa kasi na kuwa sauti ya vijana wa Tanzania. Muziki huu unaitwa “Singeli,” na ingawa ulianza kama mziki wa kihuni, sasa unafunua utajiri wa tamaduni za Kitanzania na kupelekea watu kukumbatia kwa dhati.
Jina “Singeli” lenyewe lina uhalisia wa Tanzania. Linatoka kwenye neno la Kingereza “single,” likimaanisha wimbo mmoja. Kwa kweli, awali, singeli ilikuwa mziki wa harakati za mitaani, lakini kadri muziki huu ulivyoendelea, ikawa dhahiri kuwa ni zaidi ya wimbo mmoja, bali ni sauti ya kizazi kipya cha Tanzania.
Watu wengi wanafikiria kwamba singeli inawakilisha Tanzania kuliko aina nyingine yoyote ya muziki. Hii ni kwa sababu, licha ya awali kuonekana kama mziki wa vijana wa mitaani, singeli imegeuka kuwa sauti ya taifa, ikitafakari maisha na changamoto za Watanzania wa kawaida.
Mwaka wa 2010, vijana wa Tanzania, walianza kuingiza mashairi ya kiswahili katika nyimbo zao za singeli. Hii ilikuwa hatua muhimu katika kutoa ujumbe wa utamaduni wa Kitanzania kupitia mziki. Wasanii kama Msaga Sumu, Sholo Mwamba, Man Fongo, Sisko Kiduku, DJ Marota, DJ Mrisho, na wengine wengi walichangia kwa kiasi kikubwa kuendeleza singeli na kuwaunganisha watu.
Hivi karibuni, singeli imevuka mipaka ya Tanzania. Kupitia mtandao, watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamesikia na kupendezwa na muziki huu. Wimbo wa “Do Let Me Go” uliowekwa na Mc Kinata na Ibrah ni mfano mzuri wa jinsi singeli inavyopendwa hata nje ya nchi.
Singeli pia imekuwa ikivuta wasanii kutoka muziki mwingine, kama Bongo Flava. Kwa kuwa inakua kwa kasi na kuwa sauti ya vijana wa Tanzania, hata wasanii wa Bongo Flava wamevutika na kuomba kushirikiana na wasanii wa singeli kwa matumaini ya kupata msisimko wa nyimbo zao.
Na bila shaka, wasanii wengi wa singeli wamejitokeza katika eneo hili la muziki. Wasanii kama Fighter Kidene, D Voice, DJ Auto Run, DJ Kibinyo, DJ Duke, DJ Joba, DJ Mapoda, Virus MC, Kiluza Fanani, Mdogo Elisha, MC Zo Mofan, MC Balaa, Meja Kunta, Seneta Kilaka, Dox Classic, Dulla Makabila, na wengine wengi wamefungua milango mapya na kuupa nuru mziki wa singeli.
Singeli sio tu mziki wa leo wa Tanzania, bali ni sauti inayosambaa haraka duniani. Kasi yake ya usambazaji imekuwa ya kuvutia, na hii inaashiria kuwa singeli inaweza kuwa mziki mkubwa sana duniani. Ikiwa utaipenda au kuitaja kama mziki wa vijana, ukweli unabaki pale kwamba singeli ni sauti ya Tanzania, na sasa, sauti hii inapenyeza mipaka na kuenea kote duniani, ikiwaleta watu pamoja kwa njia ya muziki.
#KonceptTvUpdates