Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) imetahadharisha wananchi juu ya uwepo wa Mvua za El Nino ambazo zinatarajiwa kuanza Oktoba hadi Disemba katika msimu wa mvua za vuli nchini zinazoelezwa kusababishwa na joto kali katika Bahari ya Pasifiki ambazo hupelekea uwepo wa mvua kubwa au joto kali kama linaloendelea kwa sasa barani Ulaya na Marekani.
Utabiri huo wa TMA wa mvua za vuli, unatarajiwa kuwa juu ya wastani hadi wastani katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na ukanda wa Ziwa Victoria, pamoja maeneo ya machache ya Mashariki mwa Ziwa Victoria ambazo zitakuwa na vipindi hivyo vya mvua.
Akieleza hayo mbele ya waandishi wa habari leo Agosti 24 Dar es Salaam wakati akitoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli 2023, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Ladislaus Chang’a, amesema mvua za vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023.
Mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria ambako kunaelezwa kutakuwa na mvua hizo, ni pamoja na Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.
Pia Dk Chang’a amesema ukanda wa Pwani Kaskazini utajumuisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Kisiwa cha Mafia, Dar es Salaam, Unguja na Pemba pamoja na Tanga ambapo mikoa yote inatarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani.
Ametaja kuwa Nyanda za juu Kaskazini Mashariki zinahusisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro ambapo inatarajiwa kupata mvua wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Oktoba na kutamatika wiki ya pili ya Januari 2024.
Kufuatia utabiri huo, Dk Chang’a ametoa tahathari kwa wakulima kutokana na uwepo wa unyevunyevu unaotarajiwa kuathiri ukuaji wa mazao.
Hivyo basi, wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda na kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati kutokana na magonjwa kama vile ukungu ambao huathiri mazao.
“Kwa upande wa Afrika Mashariki hali hii huambatana na ongezeko la mvua japo si mara zote na hii ni kwasababu inategemeana na mifumo ya hali ya hewa katika bahari ya hindi na sehemu nyingine,” amesema.
#KonceptTVUpdates