Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wamiliki wa mabasi kuzingatia Utunzaji na Uhifadhi wa mazingira kwa kuweka vyoo na vitenganishi taka kwenye mabasi yao wanapokuwa safarini na kuacha Tabia ya kuwashusha abiria kwenye maeneo ya misitu kwa ajili ya kujisaidia (Kuchimba dawa) ifikapo oktoba 2 na yeyote atakaye kamatwa akifanya kitendo hicho atapigwa faini isiyopungua kiasi cha shilingi millioni 5 pamoja na kufutiwa Leseni.
Agizo hilo limetolewa leo Agosti 31,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Mafwenga Gwamaka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na abiria kwenye mabasi pamoja na namna sahihi ya kudhibiti uchafuzi huo katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa NEMC Dar es Salaam.
Amesema abiria wa mabasi wamekuwa chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira kwa kutupa taka madirishani na kuchimba dawa mapolini wakati wa safari ndefu hali inayopelekea kuhatarisha maisha yao pamoja na kuchafua mazingira hasa vyanzo vya maji.
“Kumekuwa na tabia ya abiria kutupa mabaki ya vyakula madirishani popote pale, au kwenda haja kubwa na ndogo wakati wa safari ndefu, barabarani huko kuna hifadhi za misitu, kuna mbuga za wanyama, kuna hifadhi barabara zote hizi zinatakiwa kulindwa, kwa maana hiyo hii sio nzuri kwanza ni kuchafua mazingira, lakini pia ni kuathiri afya, na kubwa zaidi ni kudhalilisha wanawake” amesema Dkt. Gwamaka.
Amesisitiza kuwa uchafuzi aina hii una athari kubwa katika mazingira kwani huibua magonjwa ya mlipuko, husababisha kuchafuliwa na kuziba kwa vyanzo vya maji hupelekea mikondo ya maji kuziba, husababisha mchafuko wa hali ya hewa pamoja na kuharibu ikolojia ya wanyama na mimea.
Amezitaka Halmashauri kote nchini kwa kushirikiana na TABOA pamoja na LATRA kuhakikisha elimu ya utunzaji wa mazingira inatolewa na kujenga vyoo maeneo husika ili kuepukana na adha hiyo ya uchafuzi wa Mazingira.
#KonceptTVUpdates